ZITTO KABWE :HIZI NDIZO NJIA ZA RAIS KUWA DIKTETA


Na Zitto Kabwe

1 Chaguliwa kuwa Rais Hakikisha kwanza unakuwa na mamlaka ya dola vizuri zaidi kwa kuchaguliwa kwa kura. Adolf Hitler wa Ujerumani alihitaji chama chenye nguvu kumwezesha kuwa Kiongozi wa Ujerumani. Huwezi kuwa Kiongozi wa Imla bila ya kuwa na nguvu za dola. Vladimir Putin amekuwa akichaguliwa kila wakati na hata alipomaliza muhula wake aliweza kuweka mtu wa kumshikia nafasi kwa muda na kurudi tena.
2 Weka mazingira ya Udharura Udharura unaweza kuwa nafasi kwa Mtawala anayetaka kuwa dikteta kutekeleza nia yake hiyo. Udharura unasaidia kutunga sheria ambazo zinampa nafasi Rais kufanya maamuzi bila kutegemea vyombo vingine. Aghalabu anayehoji maamuzi hayo huitwa si mzalendo, msaliti, mhaini nk. Hitler wa Ujerumani alituma vijana wake kuwasha moto jengo la Bunge ili kuweka udharura. Alilaumu wakomunisti kuwa ndio wamechoma moto jengo hilo na hivyo kuanza kuwashughulikia. Nchini Burundi, Pierre Nkurunzinza aliamua kufanya mapinduzi bandia ili aweze kutekeleza nia yake ya kukaa kwenye madaraka daima. Baadhi ya Watawala huanzisha ajenda za ‘ kizalendo’ ili kuweka udharura. Ajenda hizo ni kama vile tishio la kuvamiwa na nchi nyengine, tishio la kuporwa mali zao asili nk. Mtawala Dikteta hutangaza vita zake binafsi na kuzifanya ni vita za kitaifa na yeyote anayehoji ama umuhimu wa vita hizo au namna zinavyoendeshwa hushughulikiwa na hata kupotezwa.
3 Pitisha sheria ya Hali ya hatari Kukiwa na sheria ya hali ya hatari katiba ya nchi inasimama na nchi inaendeshwa kwa amri za Rais. Hapa Mtawala Dikteta anakuwa amepata fursa ya kutenda yale tu anayotaka yeye. Kwa baadhi ya nchi za Kiafrika hili halihitajiki sana. Rais anaweza tu kusema tupo kwenye vita Fulani na baadhi ya sheria kusimamishwa nan chi kuendeshwa kwa Amri ya Rais, halali ama batili.
4 Chezea Uchaguzi Hapa Dikteta anaamua kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika na yeye kushinda. Atahakikisha kuwa anabana vyama vingine kukua kwa kufunga viongozi wake au kuhakikisha wanakimbilia uhamishoni, wapiga kura watateswa na kulazimishwa kupigia kura Dikteta huyo na hata matokeo kutangazwa kutokana na matakwa ya Dikteta. Hapa Afrika, watawala wengi wamekuwa wakifanya hili bila woga. Uganda, Rwanda, Zambia, Zimbabwe na Angola imeshuhudia chaguzi za namna hii hata kama baadhi ya nchi watawala wake sio Madikteta haswa, ama ni madikteta uchwara au ni madikteta mamboleo.
5 Pitisha sheria kandamizi Sheria zinazohusu uhuru wa vyombo vya habari huwa ni za kwanza kuanza kubadilishwa ili kuziba uhuru wa mawazo na fikra mbadala. Kisha sheria zinazotoa uhuru wa vyama vya siasa na vyama vya kijamii hasa asasi zisizo za kiserikali ( NGO ) huathirika.

 

6 Pitisha sheria wezeshi Hizi sheria huwezeshwa na sheria nyengine ambazo zaweza kupelekea chama tawala kuwa chama pekee kiuhalisia kwenye nchi husika. Viongozi wa vyama wataishia lupango kwa makosa kama uhaini ili kuhakikisha kuwa vyama vinakosa viongozi na hivyo kutokukua.

 

7 Futa kabisa Upinzani Hatimaye mtu yeyote wa upinzani huuwawa. Wakati hilo linatekelezwa mihimili mingine ya Dola huminywa ili kubakiza mhimili mmoja tu kutawala. Mhimili wa kutunga sheria huwekwa mfukoni mwa Mtawala na kuwezesha kupitisha sheria wezeshi. Mhimili wa mahakama hufuata maagizo ya mtawala kuhusu kesi mbalimbali zinazofikishwa mbele yake. Lengo ni kuhakikisha kuwa sio Upinzani wa siasa tu unaofutwa bali pia upinzani wa mihimili. Wabunge wasiowatiifu huuwawa, majaji wasiofuata maagizo humalizwa.
8 Jitangaze kuwa wewe ni Mtumishi wa Mungu Mtawala Dikteta hujiita kuwa yeye ni mtu wa Mungu na hutaka kuombewa kila mara. Hujiona ni mtume na yote afanyayo anatumwa na Mungu. Nani atamhoji Mungu?