IKUFIKIE HII KUTOKA KWENYE MEZA YA MBUNGE WA NZEGA MJINI MH BASHE.

Naomba nichukue fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kufanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri.

Mabadiliko haya hayajaleta tu taswira mpya juu ya watu bali Muundo wa Baraza na kuongeza ufanisi wa utendaji wa majukumu ya kila wizara.
Maamuzi ya Rais kuigawa Wizara ya Kilimo, Chakula, Ushirika Uvuvi  na Mifugo na kufanya kuwa Wizara mbili pamoja na kuigawa  Wizara ya Nishati na Madini na kuweka Wizara mbili nako kuteleta ufanisi na tija katika utendaji kwa kuongeza “URAHISI WA KUFIKIA MALENGO” kwa kuziwezesha Wizara hizi kuweza kutekeleza malengo mahsusi (Specific Objectives) bila ya kutoka nje ya mstari(focus) au kwenye malengo makuu.
Ajenda ya Serikali ya Awamu ya Tano iliyo chini ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli imekua ni kujenga Taifa la Viwanda na kufikia malengo ya Uchumi wa Kati.
Msingi mkuu wa Viwanda ni Rasilimali watu, Malighafi na Nishati. Kwa ajili ya matokeo sahihi na yenye tija vitu vyote hivi lazima viwepo na kutumika kwa ufanisi ili kuleta matokeo sawia.
Kilimo pekee kwa mujibu wa takwimu za sasa kimeajili zaidi ya asilimia 65 (65%) ya watanzania; Hivyo uwepo wa Wizara ya Kilimo peke yake na uwepo wa wizara ya Nishati peke yake utajenga msingi mkubwa wa kusukuma kwa kasi maono yetu ya kuwa taifa la Viwanda.
Hivyo; Maamuzi ya Rais ya kuzigawa wizara hizi ni maamuzi ya kimkakati; maamuzi ya kupongezwa na kuungwa mkono kutokana na mahitaji ya Taifa kwa sasa.
Aidha, Baraza hili limekua na mchanganyiko wa wazee na vijana lakini pia kumekua na ongezeko kubwa la wanawake hivyo kupanua nafasi ya ushiriki wa wanawake katika maamuzi na maendeleo katika ngazi ya Taifa.
 Ni kawaida katika uendeshaji wa serikali kwa Rais kufanya tathmini kila baada ya kipindi fulani ili kuangalia namna bora ya kukuza utendaji na kuimarisha mahali ambapo panaonekana pameyumba kwa maslahi makubwa ya Taifa ili kufikia Malengo ya Watanzania
Hivyo maamuzi haya yamejenga Ari  mpya na mtazamo mpya wa namna ya kutekeleza mipango ya serikali ambayo itapelekea kufikia na kutimia kwa ndoto za Watanzania na dhamira ya Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Mwisho; 

Kwa dhati kabisa nawapongeza Mawaziri na manaibu wote walioteuliwa kwani Baraza hili limebeba matarajio makubwa   katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi (2015-2020) na ndio ambalo litafanikisha ushindi mkubwa katika uchaguzi ujao.
Ninawatakia Mawaziri wote na Manaibu waziri kila la kheri na utendaji mwema katika majukumu mliyopewa na kuaminiwa na Mheshimiwa Rais; na sisi kama wabunge wa Chama cha Mapinduzi wajibu wetu ni Kuwashauri, Kuwasaidia na kuwakosoa ili muweze kutembea katika njia sahihi itakayoweza kumsaidia Rais kufanikisha na kufikia maono ambayo ndio msingi wa serikali yetu.
Mungu Ibariki Tanzania,

Mungu Wabariki Watanzania.
Hussein Mohammed Bashe (MB)

Nzega Mjini

10 Oktoba 2017