TUTEGEMEA KUIONA BARCELONA KATIKA LIGI KUU YA UINGEREZA MSIMU UJAO??

Na: Pasco Nkololo.

Imeripotiwa kwamba klabu za Barcelona, Espanyol na Gerona zinaweza kujiunga na ligi ya uingereza, italia au ufaransa endapo mpango wa kura ya maoni ya wananchi wa Catalunya utafanikiwa na kuifanya Catalunya kujitenga na nchi ya Spain.

Mtandao wa Goal.com umemnukuu waziri wa michezo wa Catalan bwana Gerald Fegueras akieleza namna vilabu kutoka Catalan vitakua na nafasi ya kuchagua ligi ya kushiriki endapo hawataridhishwa na mazingira ya Catalan katika kipindi hiko cha mpito.

Kura hiyo ya maoni ya wacatalan kujitenga na Uhispania inatarajiwa kupigwa mapema siku ya jumapili tarehe 31 September ambapo waziri huyo haoni kama kunaweza kuwa na uvunjifu wowote wa sheria na kanuni za soka kwa mujibu wa shirikisho la soka la ulaya UEFA kwa timu moja kushiriki ligi ya nchi nyingine kwani si jambo geni katika soka la ulaya.

Akitolewa mfano wa timu kama Swansea ambayo ni mfano wa timu kutoka wales ambayo inashiriki ligi ya England pasi na kuathiri sheria za UEFA.

Mpaka sasa klabu ya barcelona haijalizungumzia suala hilo ikiendelea na ratiba zake za kimashindano kama kawaida huku ikiwa na rekodi ya ushindi mfululizo wa mechi nane tangu ianze kunolewa na kocha mpya Ernesto Valverde.

Kwa upande wa rais wa La liga bwana Javier Tebas amekua akinukuliwa mara kadhaa akisisitiza kwamba kwa namna yoyote utengano wa wacatalunya kutoka Hispania utakua na athari za moja kwa moja kwa ushiriki wao katika ligi kuu ya Hispania maarufu kama La Liga na hivyo kutoa uwezekano wa maneno ya Gerald Gegueras kuweza kutimia na kuzishuhudia team za Barcelona na Espanyol katika ligi kuu ya Uingereza.