TUNAWEZA LIVE ZA RAIS KWANINI TUSHINDWE BUNGENI NA MAHAKAMANI

NA EGBERT MKOKO

AGOSTI nane, Jumanne ijayo, umma wa Afrika Kusini utakuwa ukitazama kwenye runinga ya Bunge la nchi kupitia king’amuzi cha DSTV, ama katika chaneli maalumu ya ‘SABC News’ inayopatikana katika king’amuzi hiki pekee, kushudia upigwaji wa kura ya kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma.

Chaneli hizo mbili huonyesha moja kwa moja matangazo ya Bunge la Afrika Kusini na hata baadhi ya vikao vya kamati za bunge hilo.

Ni jambo la kawaida kwa Bunge la Afrika Kusini kuonyeshwa mbashara kila mara kwa chaneli nilizozieleza hapo juu, licha ya kwamba runinga nyingine hujiunga na kuonyesha mbashara matangazo ya bunge kunapokuwa na hoja nzito inayojadiliwa na hasa ile inayohusu mustakhabali wa taifa. Hoja ya kutokuwa na imani na Rais Zuma ni nzito na inahusu mustakhabali wa taifa na hivyo upo uwezekano hoja hiyo ikaonyeshwa na runinga nyingi zaidi ya hizo mbili nilizozitaja hapo mwanzo.

Bunge ni mmoja kati ya mihimili inayoongoza nchi yoyote ile duniani ikungana na Mahakama pamoja na Serikali au dola. Bungeni ndiko kuna uwakilishi mpana wa wananchi tofauti na ilivyo katika serikali ama ilivyo mahakamani. Nchi nyingi kama Afrika Kusini na hata jirani zetu Wakenya, hutumia moja ya chaneli katika runinga za umma ili kuwapa wananchi ile haki ya kupata habari inayoainishwa ndani ya katiba.

Ni bahati mbaya sana sisi Tanzania ambao tulikuwa tumepiga hatua kubwa na kufika mbali katika haki ya wananchi kupata habari na hasa zile zinazohusu Bunge, sasa tumerudi nyuma kutokana na uamuzi uliochukuliwa na serikali ya sasa juu ya matangazo ya Bunge. Sina haja ya kurudia kuelezea ubaya wa uamuzi huo na athari zake kwa wananchi kwani mengi yalikwishakuelezwa.

Wakati mhimili wa Bunge ukipewa nafasi hiyo kwa wananchi kushuhudia moja kwa moja matangazo kutoka ndani ya chombo hicho, wenzetu Afrika Kusini wamepiga hatua moja mbele zaidi. Shughuli za Mahakama nazo hupewa nafasi ya kuonyeshwa mbashara katika runinga kadhaa.

Kesi kubwa na zile ambazo zinavuta hisia za wananchi wengi wa Afrika Kusini, hupewa fursa ya kurushwa mbashara na runinga za nchi hiyo bila wasiwasi. Kama ilivyo ada, runinga ya umma ya SABC News hurusha moja kwa moja kesi zote ambazo zina mvuto ama zinagusa hisia za watu wengi.

Mahakama za wenzetu hazioni tabu kuonyeshwa kwa shughuli zake kwa uwazi kwani hakuna jambo la kificho na tafsiri ya kisheria hutolewa kwa uwazi bila kuficha chochote. Tafsiri hiyo ya kisheria haimaanishi kwamba mwenye haki ndiye atakayeshinda, la hasha. Atakayeshinda kesi ni bingwa wa kutafsiri sheria bila kujali kama una haki au lah. Hiyo ndiyo kazi ya Mahakama.

Zipo kesi nyingi ambazo zimewahi kurushwa moja kwa moja na watu wengi kushuhudia iwe ndani ama nchi ya Afrika Kusini. Mfano mzuri ni kesi ya mauaji iliyokuwa ikimkabili mwanariadha mlemavu Oscar Pistorius. Kesi ile ilikuwa ikirushwa mbashara tangu ilipoanza hadi ilipomalizika. Kwa bahati mbaya sana, jambo hili ni geni kwa Mahakama ya Tanzania.

Mhimili ambao umekuwa ukipewa nafasi kubwa Tanzania katika shughuli zake kuonyeshwa mbashara ni serikali au dola. Kwa wiki kadhaa, Watanzania wamekuwa wakishuhudia shughuli mbalimbali za Rais John Magufuli katika maeneo kadhaa kuanzia Chato hadi Dodoma na Dar es salaam.

Tayari sasa imekwishakutangazwa kwamba Agosti tano mwaka huu, wananchi watashuhudia mbashara shughuli ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bomba la mafuta toka Tanga hadi nchini Uganda, shughuli itakayohudhuriwa na Rais Magufuli na mgeni wake Rais Yoweri Museveni wa Uganda. Walau katika eneo hilo, tunafanana na wenzetu wa Afrika Kusini.

Kinachotutofautisha hapa ni uwazi katika shughuli za Bunge na Mahakama. Ikumbukwe kuwa vyombo ama mihimili hii mitatu inapaswa kufanya kazi bila kuingiliana, kila kimoja na uhuru wake wa utendaji kazi.

Bunge letu ambalo ni chombo chenye uwakilishi wa wananchi, hakiweki wazi shughuli zake kama ilivyo kwa Rais ambaye ni mkuu wa mhimili wa Serikali. Mahakama vivyo hivyo, shughuli zake haziko wazi katika runinga zaidi ya kusubiri taarifa ya habari ya saa mbili usiku. Wenzetu wamepiga hatua zaidi katika maeneo haya.

Licha ya kwamba tumerudi nyuma katika ile haki ya kupata habari za Bunge ikilinganishwa ilivyokuwa mwaka 2015 na sasa 2017, lakini ipo haja ya kujifanyia tathmini ikiwa tuko katika mwelekeo sahihi ama tunapaswa kufanya mabadiliko na kuiboresha haki hii ya mwananchi kupata habari.

Jirani zetu Kenya wamepiga hatua kiasi kwamba hata usaili wa waombaji wa nafasi kubwa serikalini ama katika Mahakama, huonyeshwa mbashara na wananchi hupata nafasi ya kuona uwezo wa waombaji wa nafasi hizo.

Sina hakika kama mjadala ulishafungwa na naamini serikali ya Tanzania ni sikivu na yenye kutafakari mambo kwa kina. Ni wakati muafaka Mahakama ya Tanzania kutafakari na ikiwezekana kubadilika na kuzipa nafasi runinga kuonyesha mbashara mwenendo wa kesi mahakamani zile ambazo zinavuta hisia za wananchi wengi.

Aidha, Bunge nalo (serikali?) itafakari upya uamuzi wa kupunguza muda wa kuonyesha mbashara matangazo ya Bunge kama ilivyokuwa zamani. Kwakuwa matangazo mbashara ya shughuli za serikali hayajaleta athari zozote katika utendaji kazi wa serikali na badala yake kuweka uwazi zaidi wa shughuli zinazofanywa na serikali, vivyo hivyo matangazo mbashara ya Bunge na Mahakama yatakuwa fursa nzuri kwa Mtanzania kujua namna vyombo hivyo vinavyotenda kazi zake iwapo ni kwa haki kweli ama kuna walakini