TUNAISHUKURU SERIKALI KWA KUENDELEA KUTATUA KERO YA MAJI NZEGA MJINI- MH.BASHE

Na John Marwa
Mbunge wa Nzega Mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Mh. Hussein M. Bashe, amemshukuru Rais John Pombe Magufuli kutokana na namna ambavyo amekua mstari wa mbele kushirikiana nao kutatua kero kubwa ya maji katika Jimbo la Nzega Mjini.

Mh.Bashe alisema kuwa, hivi karibuni akiwa kwenye ziara jimboni kwake, alipata heshima ya kutembelewa na Waziri wa Maji Mh.Mhandisi Kamwele ambapo kwa pamoja walipata wasaa wa kukaa pamoja na timu ya wataalamu wa wizara kujadili utekelezaji wa Mradi wa maji ya Ziwa Victoria unaoendelea kwa sasa.

Alisema, kwa kina waliweza kujadili mapungufu yaliyojitokeza na mahitaji halisi.

“Nitumie fursa hii kuishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa jitihqda hizo,” alisema.

Aidha, katika majadiliano hayo alimueleza Mheshimiwa Waziri mapungufu makubwa ya maji kwenye maeneo ambayo Mradi hautafika ambapo pia kipekee ameishukuru kwa dhati Serikali kwani walifikia muafaka kutatua changamoto hiyo kwa kuanza Utekelezaji wa Mradi mkubwa wenye thamani ya pesa za kitanzania Bilioni Moja (Tzs 1,000,000,00).

Aliongeza kuwa, mradi huo unaohusisha upanuzi wa miundombinu ya maji kwa maeneo ambayo hayatafikiwa na Hatua ya Kwanza Maji ya ziwa victoria.

Pamoja na hilo pia watachimba visima virefu 13 vya kutumia Teknolojia ya nishati ya Jua (Solar energy).

Alifafanua kwa kusema kuwa, visima hivi vitahudumia maeneo ambayo Mradi wa maji ya ziwa Victoria hautafika kama ifuatavyo;
(a) Kijiji cha Nhobola – visima 2
(b) Kijiji cha Igilali – Visima 3
(c) Kijiji cha Iyuki – Visima 2
(d) Kijiji cha Kitengwe – Visima 2
(e) Kijiji cha Idudumo – Visima 2
(f) Kijiji cha Mwanzoli – Visima 2.

Kwa muda mrefu maji yamekua ni changamoto kubwa sana katika Jimbo la Nzega Mjini na Nzega kwa ujumla lakini hatua hii ni muhimu na tayari tenda ya visima 13 imeishatangazwa.

“Narejea kumshukuru waziri kwa kupita katika Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini na pia namshukuru kwa jitihada zake binafsi  alizoonyesha kukutana na Wataalamu wa Maji wa Halmashauri ya mji wa Nzega, nimuhakikishie waziri kuwa, mradi huu tutausimamia kikamilifu kwa ajili ya mafanikio na matokeo yaliyokusudiwa na kuwa mfano wa miradi mingine mingi ya Maji nchini” alisema Mbunge huyo.

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*