TUMUAMINI NANI, CHADEMA AU ZITTO KABWE?

Kutoka mezani
Kwa

Habib Mchange

TUMUAMINI NANI, CHADEMA AU ZITTO KABWE?

Na. Habib Mchange

Kwa kipindi cha siku kadhaa sasa tumekuwa tukishuhudia maneno makali kutoka kwa wanachama na viongozi wa Chama cha Chadema kwenda kwa kiongozi wa chama cha ACT WAZALENDO ndugu Zitto Kabwe.

Njia mbalimbali zimetumika kufikisha mashambulizi hayo huku mitandao ya kijamii ikishika hatamu sambamba na makala za magazetini wakimuita Zitto kabwe ni Msaliti, wengine Kinyonga na wengine Mamluki huku Leo nikisoma makala nyingine ikimuita Zitto Kabwe ni Uyoga kwamba uyoga unaweza kutumiwa kama chakula na kadharika sumu.

Licha ya wanachama na viongozi hawa kujisahau pengine kuwa Zitto sio mwanachama wa chama chao na kwamba yeye ni mwanachama wa chama kingine kinachojitegemea chenye Sera, katiba na miongozo yake, lakini ni Dhahiri Viongozi na wanachama wa Chadema hawawezi kumsahau Zitto Kabwe.

Kama kuna jambo Chadema na viongozi wake nahisi linawauma na kuwanyima usingizi, basi kuendelea kuwepo kwa mwanasiasa huyu waliyemfukuza chama chao kwa matusi na kejeli nyingi mwaka 2015 mwanzoni.

Naam, ukisoma makala na maandiko yanayomdhambulia Zitto kisa tu kakosoa kauli ya mwanasheria wa chama cha Chadema Tundu Lissu kuhusu kutaka nchi inyimwe misaada na ushirikiano wa kimataifa, hauna utakachojifunza dhidi ya Chuki dhahiri za wanachadema kwa Zitto.

Kwa Lugha nyepesi tu unaweza ukasema Chadema na wafuasi wake wanatamani sana Madini yanayotemwa na Zitto Kabwe wa ACT WAZALENDO yangekuwa yanatemwa Hata kwa asilimia 20 na mmoja kati ya wabunge wao, ndio maana Hata Zitto afanye jema lipi, Chadema wao wataacha kulijadili alilolifanya watamvaa Zitto, huu ni udhaifu wa kiwango kikubwa sana.

Chadema wameumia sana Zitto kumsifia Rais Dkt Magufuli pale Jukwaani Kigoma, imewauma kwa sababu Hawakujua kuwa Zitto hakumsifia tu Rais Magufuli, Bali pia Zitto amempongeza kwa dhati kiongozi wa nchi anayepeleka mbele maendeleo ya wana kigoma.

Wamekasirika kwanini Zitto aliwahi kuukosoa utawala wa Rais Magufuli hapo nyuma halafu juzi eti amempongeza na kuona kwamba Zitto ni kigeugeu, walitamani Zitto aendelee kukosoa tu na kupinga hata maeneo dhahiri, ama wamesahau kwamba chama alichopo Zitto kwa sasa sio kazi yake kupinga kila kitu, na ndio maana wameamua kujitanabaisha na Slogan ya Taifa kwanza wakimaanisha kuwa wao maslahi ya nchi kwao ni kitu cha msingi kuliko chochote.

Wamesahau kwamba moja kati ya vichagizo vya Zitto na chama chake ni Kuupinga ujinga popote ulipo bila kujali chama cha anayefanya huo ujinga?. Ni vigumu sana kumuelewa Zitto kama haujui mpaka unaingia kwenye chama cha siasa unataka nini zaidi ya kupinga.

TUWAAMINI CHADEMA?…

Kwa msingi wa hoja zao kuwa Zitto ni kigeugeu na kwamba haaminiki Leo anaweza akapinga jambo na kesho akageuka, nadhani CHADEMA ndio wanaongoza kwa kuwa na sifa hiyo.

Kama hiyo ndio Hoja, basi Kwa sasa, Chadema ndio chama ambacho hakipaswi na hakiwezi kuaminiwa Mara 1000 zaidi kulinganisha na Zitto alivyo.

Nitatoa mifano Michache.

Mwaka 2013/2014, Freeman Mbowe akiwa kiongozi wa upinzani na mbunge wa Hai, aliwaongoza wabunge wenzake kupinga bajeti ya wizara ya Ujenzi iliyokuwa ikiongozwa na Dkt. Magufuli, mbowe aliipinga bajeti hiyo na kupiga kura ya hapana pale Bungeni, na kusema hawezi kuunga mkono serikali ya CCM.

Mungu si Athumani, mwaka huo huo Dkt Magufuli akaenda jimboni kwa Mbowe Hai, kisha au kabla alikwenda jimboni Rombo kwa Joseph Selasini, huwezi amini aisee,

Sifa alizozipolomosha Mbowe kwa Magufuli na Kikwete (aliyekuwa Rais) hazifikii hata Robo ya zile alizozitoa Zitto Kigoma, ndio maana ilimbidi mpaka Magufuli achukue link ya YouTube na kwenda nayo Bungeni katika bajeti iliyofata na kuwaambia wabunge na watanzani jinsi serikali ya CCM inavyochapa kazi kiasi cha kusifiwa hadharani na Freeman Mbowe. – NANI Tumuamini sasa, Chadema au Zitto?.

Naongeza, Kabla ya tarehe 15-09-2007, msamiati wa neno FISADI haukuwa maarufu hapa nchini Tanzania.

Unamjua aliyeuibua sawa sawa?.

Ni Chadema kupitia Tundu Lissu,

Ndio, Tundu Lissu akiwa Mwanachadema na mwanasheria machachali, tarehe 15-00-2007 pale viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es salaam, akishirikiana na Mbowe, na viongozi wengine wa upinzani akiwemo Dkt. Slaa, Maalim Seif , Mbatia na Wengine. Lissu alisoma Orodha ya Watanzania kumi na moja wanaolifilisi Taifa hili la Tanzania, tena akasema watu hawa hawanastaha ya kuitwa jina lingine zaidi ya MAFISADI, Lissu akasoma Orodha ya Mafisadi akisindikizwa na vifungu kibao vya Sheria.

Katika Timu ya watu 11 waliotajwa na Lissu kama mafisadi wanaoliumiza Taifa mtu NAMBA 9 aliyetajwa na Lissu na Chadema ni *EDWARD LOWASSA* Kwamba kwa mujibu wa Lissu na Chadema LOWASSA ni miongoni mwa Wafilisi 11 wa nchi hii, Leo LOWASSA yuko wapi, na Lissu yuko wapi na anasemaje?. – Tuwaamini Chadema?.

Naongeza, Mwaka 2011/2012 kule Arumeru palikuwa na Uchaguzi wa Marudio, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema ambaye pia ni Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema, alisimama Jukwaani na Kuwashukuru wananchi kuwa walimzomea Mzee LOWASSA. Nitayarejea baadhi ya maneno yake

*”Jana mmemzomea LOWASSA, ni Heshima kubwa kwa Mungu Kumzomea Mwizi, LOWASSA ni FISADI*” Huyo ni God bless lema wa Chadema, Leo LOWASSA yuko wapi na Lema yuko wapi?, anasema nini?..- TUWAAMINI CHADEMA?.

Niongeze?… Msigwa alimtukana LOWASSA, akasema atakayemnadi na kumshabikia LOWASSA akapimwe akili yake, nani alimnadi LOWASSA 2015, ni Zitto au Msigwa?. – Tuwaamini Chadema?

Mwaka 2010 katika kampeni za Uchaguzi mkuu Moja kati ya Sera za Chadema ilikuwa ni Kurudisha viwanda vyote vilivyobinafsishwa na kugeuzwa maghala, Chadema wakasema watavirudidha kwa wananchi, Mbowe akasema lazima virudi, Leo mwaka 2017 Mbowe yule yule anasema serikali imekosea kutoa tamko la kuvirudisha viwanda vile vile walivuotaka kuvirudisha wao mwaka 2010. Tuwaamini Chadema?…

Mwaka 2010 mpaka 2013 mwanzoni, CUF waliitwa CCM B na CHADEMA, Nccr wakaitwa Washirika wa CCM, miezi michache mbele CCM B na washirika wa CCM wakaungana wakaitwa UKAWA. tuimini Chadema?

Mifano iko mingi mingi mingi sana.

USHAURI

nawashauri viongozi na wanachama wa Chadema waachane na Zitto, wajenge Chadema yao, wamuache Zitto na ugeu geu wake na chama chake, watu makini wanafahamu kwamba Chadema ni kikundi cha watu wasaka madaraka tu na sio chama cha siasa.

Chama makini chochote cha siasa hakivunji wala kukiuka misingi yake iliyojiwekea,

Chama makini cha siasa hakiwezi badili Gia angani, lakini kikundi cha wasaka madaraka kinaweza Fanya lolote lile ilimradi tu kipate madaraka.

Wamuache Magufuli afanye kazi ya kuleta maendeleo aliyoahidi, maendeleo hayana chama, maendeleo hayana dini maendeleo hayana Kabila.

Kama Zitto alimpinga Magufuli Jana, sio kigezo cha kpongeza Leo kama amefanya vizuri na wala sio kizingizi cha kutokumkosoa kesho akifanya vibaya, hiyo ndio huitwa siasa ya masuala.

Ndio maana LOWASSA hamsimangi Lissu aliyemwita Fisadi namba Tisa hapa nchini,

Ndio maana LOWASSA hamsimangi Lema aliyekesha akimtukana katika mikutano ya kisiasa

Ndio maana LOWASSA hamsimangi msigwa, hamsimangi Mbowe aliyemkejeli kuwa ni dhaifu na baadae kumpokea wala hamsimangi yeyote, anafanya siasa zenye kukipigania anachokiamini atakipata ama anataraji kukipata.

Vijana, viongozi na wanachama wa Chadema kuhangaika na kina Zitto, Kitila mkumbo na Anna Mgwira ni kujidharirisha kwa kuonyesha kiwango kidogo cha uelewa wa masuala ya siasa.

Nawapongeza sana baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema wanaojikita kila uchao kuhangaika kutafuta suluhu ya changamoto za wananchi wao kama MEYA Boniface Jacob, John Mnyika, David Silinde Mwita Waitara nakadharika.

Muhimu kujua ni kwamba Zama zimebadilika, siasa zimebadilika, siasa za Leo si sawa na siasa za miaka mitano iliyopita.

Siasa za Leo zinahitaji wanasiasa wanaoleta majawabu kwa wananchi wao kuliko kutukanana kila uchao. Mmesha tukanana imetosha sasa wapeni majawabu wananchi.

Ndimi,
Habibu Mchange
0762178678
Mwananchi wa kawaida.