TRUMP AMTAKA PUTIN AKUBALI RUSSIA KUINGILIA UCHAGUZI WA MAREKANI

Rais wa Marekani Donald Trump amemshinikiza Rais mwenzie wa Russia Vladimir Putin akubali kuwa Moscow iliingilia kati uchaguzi wa urais wa Marekani mwaka 2016.

Kauli hiyo imekuja baada ya viongozi hao kukutana uso kwa uso Ijumaa, Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson.

Tillerson amesema Putin amekanusha kuwa Russia iliingilia kati uchaguzi, japokuwa viongozi hao wawili walikuwa na “mazungumzo marefu na ya tija juu ya suala hilo.”

“Rais alimbana Rais Putin zaidi ya mara moja kuhusu Russia kuingilia kati uchaguzi wa Marekani,” Tillerson aliwaambia waandishi baada ya viongozi hao kukutana.

Mkutano wao ulivuma zaidi kuliko mkusanyiko wa G20 Hamburg, Ujerumani, uliowaleta viongozi wa mataifa 20 yenye uchumi mkubwa duniani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov, ambaye pia alihudhuria mkutano, baadae alisema kuwa Trump alikubali kauli ya Putin kwamba Russia haikuingilia uchaguzi wa Marekani.