TANZANIA YAPOKEA TRILIONI MOJA KUTOKA UINGEREZA

Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania imepokea msaada wa dola za Marekani 450 sawa na trioni moja za Tanzania kutoka Uingereza zitakazotumika kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

Akikabidhi msaada huo Waziri wa Nchi anayeshughulikia maendeleo ya kimataifa na masuala ya Afrika katika ofisi ya Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola ya Uingereza Mhe. Rory Stewart amefanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar Es Salaam.

Mhe. Rory Stewart ameeleza kua fedha hizo zitaelekezwa katika maeneo mbalimbali ya maendeleo hususani katika kuinua ubora wa elimu na kuimarisha miundombinu hasa barabara na bandari, kuinua kilimo cha kibiashara na viwanda.

Aidha, Mhe. Stewart amempongeza Mhe. Magufuli kwa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa na hatua zilizochukuliwa kuimarisha elimu kwa kuwapa nafasi Watanzania wengi zaidi kupata elimu.

Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rory Stewart kwa kuja nchini na amemuomba ampelekee shukrani zake kwa Malkia Elizabeth II na Waziri mkuu wa Uingereza Mhe. Theresa May kwa msaada mkubwa walioutoa.