AKILI INAPOUSEMEA MOYO KUPITIA MUZIKI.

Na: Ricardo Samwel


Moyo wa mwanadamu uliumbwa  kiufundi,mapigo yake 70 kwa dakika moja,kisayansi kazi ya moyo ni kusukuma  damu,lakini lipo kosa la kimantiki  kuwa Moyo pia una kazi ya kupenda.

Naam upendo ni msingi wa Mapenzi. Mapenzi anuwai,Mapenzi yenye hisia ainaaina, Mapenzi zawadi ambayo mwenyezi Mungu aliwakirimia waja wake.
Kila mtu  hupenda, Lakini hali huwaje  umpendaye anapokwenda kinyume na makubaliano yenu?Ni hisia zisizoelezeka zenye maumivu makubwa ambayo huacha makovu katika moyoni mwetu. 
Wanamuziki kama walivyo watunzi wengine wa kazi za fasihi hutumia vipawa vyao  kutufikishia ujumbe wenye mguso ndani yake.
Zipo tungo nyingi za kiswahili hasa  katika music wa bongofleva Lakini zifuatazo ni baadhi ya tungo bora zaidi zenye ujumbe wa kuonyesha hisia hasi  za kimapenzi, 
Kama ambavyo inaaminika kuwa moyo hupenda, vivyo hivyo akili huwasilisha hisia zake kupitia maneno na tungo.Tuziangalie tungo hizo

1.HAYAKUWA MAPENZIMr two{SUGU}

 

Kwa sasa ni mwakilishi wa wananchi wa jimbo la  mbeya mjini akiwa mbunge katika kipindi cha muhula wa pili.

Siku hizi anapenda  zaidi aitwe Jongwe lakini nyakati hizo aliitwa Mr Two,

Katika wimbo huu Mr two anaeleza namna ambavyo nafsi yake imeumia.Katika tungo yake hiyo kuna sehemu anasema,
`Napita mtaani mawazo tele kichwani,

  washkaji wananiuliza shemeji hajambo nyumbani,

  Ntawajibu kitu gani,nikisema tumeachana ntawapa sababu gani?,

   Wewe uliondoka tu na mpaka Leo hata hujasema kitu,

   Nami sitaki kufuata yanayosemwa na watu,wanasema wazazi wako eti kwangu waliona Future hamna kitu,

   Siwezi kuwapa lawama kwa kukutakia mema,

    Haina Nouma hatuwezi kurudisha muda nyuma na maisha yatasonga..`
Katika wimbo huu jongwe anakumbuka  pia namna ambavyo alijitoa kwa mpenzi wake Lakini mapenzi yamefikia ukingoni. 

2.HAIKUPANGWAChindo man ft Wise man

Mwenyewe anapenda  kujiitwa Umbwa,mwana hip hop kutoka Arusha,Ni ukweli ulio bayana kuwa Chindo man ni mtunzi bora wa tungo simulizi(story telling) Lakini Katika tungo hii ameeleza namna ambavyo uhusiano wake umefika  tamati lakini akitoa  pongezi nyingi kwa mwenzi wake ambaye anahitimisha naye uhusiano.
Moja kati ya beti  katika nyimbo zake ipo  mistari isemayo,

`Inaniuma roho kwamba hatuwezi kuwa wote,

Kukaa pamoja na kushea mawazo wote,

Nisamehe  coz siwezi kuwa mume wako,

Tafuta mwingine umpe Maisha yako, `
Katika kuonyesha namna anavyothamini mchango wa mwanamke huyo,Chindo man anaghani kuwa,
`Asante kwa msaada wa nguo,chakula na pesa,

Kuna kitu kimoja nataka kukwambia, 

Atakaye kuoa atafaidi dear,`
Ni wimbo wenye ujumbe uliobeba hisia Kali sana.

3.KAMA ZAMANIMwana FA ft Mandojo&Domokaya ft Kilimanjaro band(Jenje)
Waswahili husema,majuto ni mjukuu na neno ningejua  huja Mwisho wa safari.
Katika wimbo huu,Hamis  mwinjuma zao la  East Coast team(ECT)Anaonyesha  majuto yake kwa kuachana n a mpenzi wake.
Anatamani  maisha yake ya kimapenzi na mpenziwe  waishi kama zamani,
Mwana FA katika ubeti wa kwanza anasema,
`Bado sinywi pombe kama ulivyoniacha sugar,

Huwa naswali,sifungi mapenzi yamenipa ulcers,
Anasisitiza pia kuwa,

`Wananicheka ujinga kila nikiongelea mapenzi,

Mfano wangu wa kwanza ni wewe tu`
Mwana FA anakiri kuwa,hakuna mwanamke wa aina yake(Aliyeachana  nae)
Wimbo wenye ujumbe na mafunzo pia.sio vyema kuchukua maamuzi magumu bila kufikiria kwa kina.

4.WHYChiku K ft Chidy Benz

Mwanadada chiku  K aliwahi kushiriki katika mashindano ya Bongo Star Search(BSS)kisha akaibukia kwenye kundi la  La  Familia lililokuwa likiongozwa na Chidy Benz,

Katika wimbo huu Chiku  K analalamika kwanini mpenzi wake ameuacha akiwa mpweke,
Katika ubeti wa kwanza Chiku  K anaghani,

`Usiku tabu,nashindwa kulala,

Ndoto mbaya kila mara,

Mapenzi yanafanya  siku ya pili Leo sijala,`
Ni tungo ambayo imejaa hisia na ujumbe wenye mguso,katika ubeti wa pili Chidy Benz halisi atakufanya ufurahie ujumbe wa wimbo mzima.

5. WHYMakamua ft Chidy Benz

Zipo nyakati ambazo mahusiano  huvunjika na kuwaacha wenzi wakiwa hawaelewi namna ambavyo mahaba yao yamefikia tamati.

Makamua katika ubora wa kipaji chake cha uimbaji  alituachia tungo inayoishi.
Makamua katika ubeti wake wa kwanza anaonyesha  maumivu anayoyapata kwa kutanabaisha,

`Kama masaa,sekunde,dakika zingerudi nyuma,ungeweza kuona jinsi gani moyo wangu unauchoma,

Na hata kama roho yangu ingekuwa na zipu ningekufungulia,`
Anasisitiza zaidi,
`Usingizi sipati,kula sili,  silali,

Nakuwaza  wewe na siwezi kusahau mapenzi na marashi yako.`
Naam,katika kiitikio Makamua anatamani  mpenzi wake huyo wa zamani amkumbuke japo jina lake tu.

Ni moja Kati ya tungo bora sana.

6.BORA TUACHANELavaLava 

Ni zao jipya katika music wa bongofleva lakini ni kijana ambaye uandishi wake ni kivutio tosha.Lavalava ni mwandishi mahiri na wimbo huu ni mfano hai.

Hutokea unampenda  mtu  na kumvumilia  lakini yeye haonyeshi kubadilika.katika wimbo huu Mtunzi anaamua kukubali kuwa yamemshinda.

Lavalava anatanabaisha,

`Yanini kung`ang`ania nishachoka kuwekwa sub,

Siwezi ooh,na mapenzi nishaghairi,

Tena Niko tayari vipigwe vinubi kengele kwa sherehe,kinagaubaga mbele ya umati tuachane, `
Lakini anakiri kumpenda  binti huyo anayehisi kumtoa  nyongo. 
Ni tungo yenye mashairi yaliyoshiba na ujumbe wa kuonyesha masikitiko 
7.AIYOLAHarmoniza

Kipaji cha  kutambulishwa katika label ya WCB,kwa sasa anajiita Konde boy.

Mmakonde huyu katika wimbo huu alionyesha maumivu yake kwa Aiyola,

Lakini waswahili husema Mapenzi hayasusiwi,na kwa kulithibitisha hilo,

Katika ubeti wa pili,Harmoniza anaimba kuwa,
`Sitosema mapenzi basi,

Nimeumbwa na moyo,

Moyo wenye matamanio na unapenda pia,`

  

Wimbo uliomtambulisha vyema na hakika ujumbe wake ndio ilikuwa chachu.

8.NISHACHOKAHarmoniza

Ni tungo nyingine inayothibitisha uandishi bora wa tungo za kuumizwa aliojaaliwa konde  boy,
Katika wimbo huu Harmoniza anaonyesha  kuchoshwa na malumbano na Mwanamke waliyeachana 

nae,
Katika maishiri yake anatanabaisha,

`Sio kama siwezi kupata aliye zaidi ya wewe,

Ila  hii dunia najichunga sana……
Kidogo cha jasho langu ulikidharau na kukinyanyasa,

Utu thamani yangu ukasahau kisa Anasa,

Afadhali Mimi nilishakuzoea,

Dharau,Mama yangu hajakukosea..
Ni tungo yenye ujumbe wenye hisia na mafunzo.

9.NATAKA KULEWADiamondplatnmuz

Mapenzi huumiza na wakati mwingine hutia simanzi.katika wimbo huu Simba wa bongofleva anatamani  kulewa  japo apunguze mawazo,
Katika mashairi yake,analalamika kuwa,
`Mi kwa Mapenzi maskini,

Nikamvisha na Pete kwa kumuoa,

Kukata vilimi limi  vya wambeya  wanafiki wanaomponda,
Kisha akatambua kuwa,

`Kumbe mjinga ni Mimi ninayetunza wenzangu wanachukua, 

Si tuko kama ishirini,mabuzi ving`asti wengine anawahonga.`
Naam mapenzi ndivyo.

10.WAACHE WAOANEChege ft Diamondplatnumz

Utakuwa katika hali gani utakapomshuhudia mwenzi wako akifunga pingu za maisha na mtu  mwingine?
Wimbo huu unatupa picha namna ambavyo moyo huzizizima.
Chege yeye analalama kuwa amegeuka shahidi  badala ya kuwa hakimu.
Diamondplatnumz yeye analalamika kutoambiwa lakini anaongeza,
`Tena nakupa maua  wapelekee,wasije yatupa naomba wayapokee,

Na dua ntafunga niwaombee,

Awape baraka mola watoto awaletee,`
Hizo ni moja kati ya tungo nzuri na bora za bongofleva zenye kuelezea  maumivu ya Mapenzi.
Lakini Mapenzi huwa hayasusiwi,ingawa yanatuumiza lakini hatujawahi kuyachoka.