TAFAKURI YA HUSSEIN BASHE MIAKA 18 BILA MWALIMU NYERERE.

Kama Kijana na Mtanzania ambaye kwa sehemu kubwa maisha yangu yameguswa sana na Siasa pamoja na Maisha ya Mwalimu Nyerere napenda kuungana na watanzania wote pamoja na dunia kwa ujumla kwenye Kumbukumbu ya Miaka 18 bila Mwalimu Nyerere kama siku maalumu ya kumkumbuka na kuenzi mambo mema aliyotuachia na kutuasa kama taifa na ulimwengu wakati wote wa Uhai wake.

“Mwalimu hayupo nasi kimwili lakini Mwalimu Nyerere yu hai kifikra, mitazamo na falsafa”

Tulipopata Uhuru mwaka 1961 Mwalimu alisema na kufanya jitihada kubwa ya kuliambia ya kuwa “Taifa letu kuwa Uhuru wa kisiasa wa Tanzania bila kuwepo kwa Uhuru wa kisiasa wa Mataifa mengine yaliyokua yanakandamizwa na ukoloni basi Uhuru wetu haukua na maana”

Tulipopata Uhuru Mwalimu alisema hadharani na kuamini katika dhana ya “UHURU NA KAZI”.

Dhana hii ilijengwa katika UTU. Kazi ni msingi wa UTU; na Mwalimu alisema kuwa alitunga sheria za kufanya tendo la kulinda mfanyakazi kuwa ni kitovu cha kila jambo.

Mwalimu aliamini kuwa KILIMO ni UTI wa Mgongo wa Taifa letu hivyo alifahamu kuwa Taifa letu ili liweze kuendelea Sekta ya Kilimo ndio msingi Imara wa Maendeleo na hapa Mwalimu ili kuonyesha anamaanisha yale anayoyasema basi alianzisha vyama vya Ushirika na kuvipa Nguvu na Nafasi kubwa katika kusaidia kuondoa Umasikini nchini.

Mwalimu aliamini ya kuwa Uhuru wa kisiasa bila ya kuwepo Uhuru wa Kiuchumi ilikua ni kazi Bure kwa Taifa lolote duniani hivyo aliamua kutunza Rasilimali za Taifa letu na kuhakikisha kuwa Muda muafaka ukifika tutazitumia hasa pale ambapo Taifa litakua na watalaamu wa kutosha wa kuweza kusimamia rasilimali hizi na kupunguza mianya ya wizi wa rasilimali zetu kwa kisingizio cha teknlojia

Mwalimu aliamini UJINGA ni adui mkubwa anayesababisha Umasikini; na umasikini ni Msingi mkuu wa Maradhi hivyo akatangaza Maadui watatu, Ujinga ,Umasikini na Maradhi lakini hakumsahau Adui wa Nne “RUSHWA” na Mwalimu aliwahi kusema kuwa ili kudhibiti adui huyu ambaye angepelekea kukua kwa kizazi cha upendeleo na uonevu walitunga sheria kali dhidi ya Rushwa.

Mwalimu alituasa kama Taifa juu ya Kusimamia Haki na kupinga aina yoyote ya dhuluma na Woga; ili kufanikiwa katika jambo hili alitumia muda mwingi kuliasa kundi kubwa la Vijana hasa wale Vijana wa TANU Youth League na kuwaambia hakuna dhambi kama ya woga na kuangalia Dhuluma ikitamalaki dhidi ya wanyonge.

Mwalimu alichukia Umasikini hasa Umasikini wa Fikra na hakuwahi kuona kuwa Umasikini ni sifa ya Uadilifu mwaka 1995 aliwahi kusema “Hakuna umasikini mbaya kama wa Fikra”

Mwalimu aliamini katika Usawa na Haki; na alichukia aina yoyote ya Ukandamizaji na aliwahi kusema “Kukubali Ukandamizaji ni Ujinga”. Mwalimu aliamini ya kuwa Jamii ikipoteza Matumaini ni Hatari kwa Ustawi na Uhai wa Jamii husika na taifa kwa ujumla.

Mwalimu aliamini Katika dhana ya Kukosoa na Kukosolewa na aliandika Kijitabu cha Tujisahihishe, Ni dhana pana ambayo inatoa fursa ya kujitathimini ili kuweza kuboresha pale panapopungua na kuongeza jitihada zaidi pale panapoonekana kuna uhai na tija.

Mwalimu aliamini katika Uongozi wenye kuheshimu Watu na Utu; katika kuhakikisha haiishi tu kusema aliamua kujenga dhana ya Uongozi badala ya dhana ya Utawala na kusema wazi kuwa msingi mkuu wa Uongozi ni Watu.

Leo 14 Oktoba 2017 tunamkumbuka Mwalimu kama Baba na Muasisi wa Taifa ambae hatunaye kimwili lakini tunae na tutaendelea kuwa nae kifikra ndani ya Kizazi kilichopo na vile vizazi vingi vijavyo kwani Mafundisho, Maono na Mitazamo ya Mwalimu inaishi na ni Hai Jana, Leo na Kesho.

Mwalimu atabaki kuwa Mtanzania aliyegusa maisha ya watanzania na waafrika wengi zaidi kutokana na namna alivyoamua kuendesha siasa zake ambazo msingi ulikuwa ni WATU na kwa kufanya hivi aliyagusa sana maisha ya watu si tu Tanzania bali ulimwenguni kote.

Wajibu wetu hasa Vijana wa Taifa hili pamoja na Watanzania wazelendo ni kuhakikisha kuwa tunasimama Imara kulinda misingi ya Umoja, Uzalendo,Haki, Ukweli, na kutokukubali aina yoyote ya Dhuluma dhidi yako ama Jirani yako ama Taifa lako; ni lazima Maslahi mapana ya Taifa letu yawe ndio mnyororo unaotuunganisha kuliko maslahi yetu Binafsi ama ya Vikundi vyetu AMA Vyama vyetu.

Maslahi ya Taifa letu ni muhimu sana kuliko maslahi na matakwa yetu binafsi au vyama vyetu.

Hekima kubwa kuliko zote ni kutambua ya kuwa sisi wanadamu tutapita, na vyama vyetu havitadumu milele ila Taifa letu litaisha milele zaidi yetu hivyo maslahi ya Taifa letu yawe mbele kuliko makundi yetu ya namna yeyote.

“Mwalimu anaishi Leo na ataishi Kesho.”

Akhsante Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kujenga misingi ya Umoja na Utaifa pasipo kuwepo Ukabila na Udini nchini. Mwalimu alitumia nguvu kubwa sana kujenga nchi ambayo utambulisho wetu uwe ni Utanzania wetu badala ya vile ilivyo leo utambulisho wetu umekua ni makundi yetu ya kisiasa, kikabila, kiuchumi na dini.

Mwalimu alijua fika ya kuwa kwa Taifa kuyaendekeza mambo haya ipo siku tutabaguana na kunyoosheana vidole na mwishowe Umoja wetu na sifa yetu ya Tanzania kuwa Taifa la kukimbilia na kisiwa cha Amani kupotea.

Tumuenzi Mwalimu Nyerere kwa yale mazuri tu aliyotukumbusha yeye mwenyewe nyakati zote za Uhai wake na tuyafuate hayo kwa gharama zote LAKINI yale mabaya tusiyaendee ili kulinda Taifa letu na tusije kuonekana kicheko mbele ya mataifa mengine na vizazi vijavyo kuwa sisi tuliowatangulia badala ya kurithi mambo mema ya Baba wa Taifa tuliamua Kurithi mabaya.

Mwisho nawaombea kwa Mwenyezi Mungu waasisi wetu wote wa Taifa hili na viongozi wetu wote waliotangulia mbele za Haki na ambao bado wanaishi hivi leo ili Mungu awalipe na kuwakarimia Heri kwa mambo makubwa na mazuri waliyoyafanya katika nchi yetu.

Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu Wabariki Watanzani.