RAIS MAGUFULI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA ALIYEKUWA MBUNGE WA MPWAPWA KUFUATIA AJALI ILIYOSABABISHA VIFO KWA NDUGU ZAKE.

Siku ya leo Septemba 18, 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa aliyewahi kuwa Naibu Waziri na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mpwapwa Bw. Gregory Teu kufuatia vifo vya watu 13 ambao ni ndugu wa familia yake waliopoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea nchini Uganda.

Chanzo cha ajali hiyo kinatajwa kuwa ni kutokana na kugongana kwa basi ambalo walikuwa wakisafiria kutoka kwenye sherehe ya harusi kugongana na lori katika barabara ya Masaka nchini Uganda wakati wanarejea nchini Tanzania, siku ya jana Septemba 17, 2017 majira ya saa 4: 00 usiku na kusababisha watu hao kufariki dunia.

“Nimepokea taarifa ya vifo hivi kwa mshtuko mkubwa, nimehuzunishwa na kuondokewa na idadi hii kubwa ya watu, nampa pole Ndg. Gregory Teu kwa kufikwa na msiba huu mkubwa, nawapa pole wanafamilia, ndugu na jamaa wote walioguswa na vifo hivi.

“Nawaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema na pia nawaombea majeruhi wote wanaopata matibabu huko nchini Uganda wapone haraka na kurejea nyumbani” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amewataka wanafamilia wote kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa wao na watu muhimu waliowategemea.