POLEPOLE: MAGUFULI AMEONYESHA DIRA KUELEKEA TANZANIA MPYA.

Katibu wa itikadi na uenezi wa chama cha mapinduzi bwana Humphrey Polepole amedai kwamba hatua zinazochukuliwa na rais wa awamu ya tano Dr John Pombe Magufuli ndio dira ya utekelezaji wa maono ya chama chake kuelekea Tanzania Mpya.


Polepole ameeleza kwamba hatua hizo ni pamoja na zile zihusuzo udhibiti wa rasilimali sambamba na mapambano ya rushwa na uhujumu uchumi, sambamba na kurejesha hali ya uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa umma kuwa ndio dira ya chama cha mapinduzi kuelekea ujenzi wa Tanzania mpya.

Polepole ameyasema hayo jana wakati wa mahijiano na kituo cha televisheni cha taifa ambapo mbali na mambo mengine Polepole alieleza kwamba chama cha mapinduzi kinao wajibu wa kuwahudumia watanzania kwa kuwa ndio dhamana kilichopewa kwa kipindi cha miaka mitano na mamilioni ya watanzania.

“CCM tunawajibika kwa watu wetu na hili ndilo agano letu na watanzania, tunao wajibu wa kuyatekeleza yale tuliyoyaainisha katika ilani yetu” alisema Polepole.

Aidha Polepole amebainisha kwa undani mikakati ya chama cha mapinduzi kuelekea ujenzi wa Tanzania ya viwanda ambayo pia ni dira ya serikali ya awamu ya tano chini ya Dr Magufuli na kwamba rais amekwisha onyesha dira na hivyo ni wajibu wa chama na watanzania kuunga mkono maono na dira hiyo.