MBUNGE WA CCM ANUSURIKA KUPIGWA NA WABUNGE WA CHADEMA

MBUNGE wa Viti Maalum (CCM) Juliana Shonza, amezua timbwili nje ya viwanja vya bunge na kunusurika kupigwa na wabunge wa upinzani kutokana na kuwatambia kwamba atahakikisha Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ambaye yuko kifungoni anaendelea kusota huko.

Katika kauli yake Shonza ambaye aliongozana na Mbunge wa Viti Maalum wa CCM, Rose Tweve alizungumza akidai ataleta maoni bungeni ili Mdee aendelee kusota nje ya bunge kutokana na alichodai matendo yake anayofanya hayaendani na hadhi ya kibunge.

Bila kutarajia Shonza alikutana na jibu la Mbunge wa Mlimba, Suzan Kiwanga (Chadema) ambaye alikuwa pembeni akimtaka kuacha roho mbaya na kumuogopa Mungu kwani hata Mdee akikaa nje ya bunge hatofaidika na jambo lolote.

“Acha roho mbaya wewe ni mwanamke unafurahia vipi mwenzako akipata matatizo? kukaa kwake nje hakuwezi kukusaidia kitu ila malipo ni hapa hapa duniani “alisema Kiwanga kauli iliyoonesha kumkera Shonza hivyo kuamsha timwili

Shonza alianza kujibu ndipo baadhi ya wabunge wa Chadema waliokuwa jirani akiwemo Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea, Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekule, wakaanza kumtaka awe hekima kwa kuangalia umri wa mbunge aliyekuwa akimtolea maneno machafu.

Hata hivyo Shonza hakutaka kuelewa na badala yake aliendelea kuzungumza huku akilia ndipo Tweve na Mbunge wa Viti Maalum CCM, Zainab Vullu wakamvuta kumtoa nje ya geti la bunge huku yeye akiwataka wamuache .

“Niacheni kama wanataka kunipiga tuone, niacheni niacheni, “alizungunza Shonza huku akijivuta kutoka mikononi mwa waliokuwa wanambeba

Wabunge wa Chadema waliwasihi kina mama wa CCM kumfunza Shonza adabu ili ajue kuheshimu watu anaozungunza nao na apunguze jazba sio kutaka kugombana na watu wazima.

“Mheshimiwa Vullu mfunzeni adabu huyu binti ana matatizo makubwa haiwezekani anajibishana na watu wazima huku akitaka kupigana nao, ni aibu mnatuambia sisi tuambizane ukweli lakini huyu binti mnamuangalia anaharibikiwa “alisema Gekule

Mbunge wa Viti Maalum Upendo Peneza ambaye alikuwepo eneo la tukio alisema “Tatizo la Shonza ana mtindo wa kukurupuka na anafanya mambo bila kufikiria na amejitia aibu kutaka kupigana na watu wazima, nakumbuka mimi alishawahi kunichongea bungeni kuwa nimevaa nguo mbaya isiyoruhusiwa wakati siku hiyo hakuwa amekutana na mimi nilivyonyanyuka akashikwa na aibu mwenyewe kwani nguo yangu ilikuwa sawa “