MBOWE:MAGUFULI AMEHARIBU UCHUMI WA NCHI

JULAI 31, 2017, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alitoa tamko la Kamati Kuu ya chama hicho kuhusu kile alichokieleza kuwa ni kuporomoka kwa uchumi wa taifa tangu Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani. Yafuatayo ndiyo yaliyojitokeza – mhariri

KATIKA tamko la Kamati Kuu ya Chadema, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alitumia zaidi ripoti ya hali ya uchumi inayotolewa kila mwezi na Benki Kuu (Monthly Economic Review) kama ilivyotolewa Julai 14, 2017 na zaidi ya hapo, akarejea pia baadhi ya ripoti zingine.

Akaendelea kueleza; “BoT huchapisha tathimini ya mwenendo wa uchumi kwa kila mwezi na kila robo ya mwaka kuonesha mwenendo wa uchumi kwa mwezi husika (Monthly Economic Review) kwa kulinganisha na mwezi uliotangulia na pia mwaka uliotangulia.

Aidha kwa ripoti hizo unaweza kulinganisha hali ya uchumi ya mwaka kufikia mwezi huo husika dhidi ya hali ya miaka iliyotangulia katika kipindi kama hicho.

“Julai 14, 2017, BoT ilitoa ripoti ya mwezi Juni inayohusu tathimini ya mwezi Mei 2017. Kwa kuzingatia umuhimu wake, tumefanya uchambuzi mfupi wa ripoti hii kwa kuangalia hali ya mwaka kufikia Mei 2017 dhidi ya hali ya mwaka ilivyokuwa

Mei 2015 ikiwa ndio mwaka wa mwisho wa awamu ya nne. Ulinganisho wa hali ya uchumi Mei 2015 dhidi ya Mei 2017 ni muhimu ili kuona mwelekeo (trend) wa Hali ya Uchumi na athari zake, chanya au hasi kwa mustakabali wetu kama taifa.

Uchumi na maisha ya wananchi

Uchumi hupimwa kwa vigezo vingi. Hata hivyo, umuhimu wa vigezo husika huwa na maana kutegemea namna vinavyoathiri maisha ya wananchi. Hapa tutaangalia vigezo vichache ambavyo vina uhusiano wa moja kwa moja (direct impact) kwenye maisha ya wananchi.

Akiba ya chakula na bei zake

Kipindi cha Mei,2015, kiasi cha akiba ya chakula kwenye ghala la taifa (NFRA) kilifikia tani 406,846 ukilinganisha na tani 74,826 Mei 2017; sawa na asilimia 18.3% tu ya kiasi cha chakula katika kipindi kama hicho mwaka 2015.

Bei za jumla kwa vyakula muhimu kama mahindi, Mei 2015 ilikuwa Tsh47,163/ kwa gunia wakati mwaka huu Mei 2017, bei ya zao hilo gunia imefikia Tsh 90,149.9/ sawa na ongezeko la bei kwa asilimia 92%. Aidha bei ya mchele gunia Mei 2015 ilikuwa Tsh 162,701/ wakati Mei 2017 gunia la mchele bei ni 176,330/=. Mazao mengine yote ya chakula, yakiwamo maharage, viazi na sukari navyo vimepanda bei kwa wastani wa asilimia kati ya 40 na 60 kutegemea na msimu lakini trend (hali) imekuwa ni kupanda tu.

Sekta ya kilimo imekua kwa asilimia 1.7% mwaka 2016/17, kiwango ambacho ni cha chini kupata kutokea kwa zaidi ya miongo mitatu.

Wakati mataifa yote duniani yanasaidia wakulima kuongeza tija katika kilimo kwa kuwasaidia ruzuku ya mbolea, Tanzania ambayo asilimia 75% ya wananchi wake wanatagemea kilimo, 2015 ilikuwa 78bn wakati mwaka 2016/17 ruzuku hii ilikuwa 10bn tu.

Tume ya maji iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria 2015 kwa lengo la kuhakikisha tunaongeza kilimo cha umwagiliaji katika bajeti ya mwaka 2016/17 ilipata Tsh0 (zero) katika bajeti yake ya maendeleo.

Hali ya ukata nchini

Wakati bei zikiwa juu sasa kuliko mwaka 2015 kabla ya awamu ya tano kuingia madarakani, hali ya ujazo wa fedha imekuwa kinyume chake na hivyo kuathiri biashara, uzalishalishaji, thamani ya mali (assets kama ardhi na mali zingine).

Ujazo wa fedha katika dhana pana kwa mwaka   kwenye uchumi (M3) uliongezeka kwa asilimia 15% Mei 2015 ukilinganisha na ongezeko la asilimia 5.2% Mei 2017 kwa mwaka.

Aidha, mzunguko wa fedha kwa maana ya kiasi cha fedha katika matumizi kwa mwaka, inaonesha Mei 2015 kiliongezeka kwa asilimia 15.2% wakati Mei 2017 kilikuwa na ongezeko hasi kwa asilimia -3%. Hiki ni kielelezo cha usimamizi hafifu wa uchumi na ndio msingi wa ukata unaoendelea nchini.

Athari za kushuka kwa ujazo wa fedha na mzunguko wa fedha kwenye uchumi katika vipindi hivyo tofauti wakati kiasi cha mfumuko wa bei kikiwa na tofauti ndogo, kwa maana kutoka asilimia 5% mwaka 2015 mpaka asilimia 6% mwaka 2017 ni pamoja na zifuatazo;

Kwanza, pesa kuwa vigumu kupatikana japo inashuka thamani. Ndio maana pamoja na mwaka 2017 pesa kuwa ngumu kuliko mwaka 2015 kwa mujibu wa takwimu hizi za BoT, lakini thamani ya bei ya chakula kama mahindi na

maharage vimepanda karibu mara mbili kwa ulinganisho wa miaka hiyo miwili.

Pili, gharama ya uzalishaji kwa sehemu kubwa inabaki kuwa juu kwa sababu bidhaa za mtaji na mashine sehemu kubwa zinanunuliwa nje na hivyo bei yake haiamuliwi na hali ya ndani. Kwa sababu wateja kipato kimeshuka soko la bidhaa zinazozalishwa hushuka na kusababisha mdororo wa biashara.

Tatu, kwa sababu ya mdororo wa biashara, wafanyabiashara wanashindwa kulipa mikopo na hivyo kuongeza presha kwenye kasi ya mikopo isiyolipika (Non Performing loans -NPL). Mpaka sasa kwa mujibu wa ripoti mbalimbali mikopo isiyolipika imeongezeka kutoka chini ya asilimia 5 mwaka 2015 mpaka asilimia zaidi ya 8 mwaka 2017. Hali hii inapunguza imani ya benki za biashara kukopesha sekta binafsi.

Nne, ukata huo unasababisha kushuka kwa thamani ya asset kama ardhi, nyumba au   mashine au mitambo iliyowekwa dhamana benki kwajili ya kupata mikopo kwasababu uwezo wa watu kununua umeshuka, na ndio sababu viwanja ambavyo viliuzwa milioni 100 sasa ukitangaza bei ya milioni 50 hupati mteja. Gari au mashine ambayo mwaka 2015 ungeuza kwa milioni 50 leo huwezi kupata nusu yake kwasababu ya ukata.

Tano, uwezo wa serikali na watu kujitegemea unapungua kwa sababu wigo wa makusanyo unapungua kutokana na biashara nyingi na ajira kupotea. Kwa sababu serikali inahitaji mapato kujiendesha na biashara zinapukutika, ni wazi mvutano wa serikali na wafanyabiashara huongezeka.

Sita, ni kwa sababu hiyo, maamuzi ya kisera na kisheria ya kushinikiza kampuni za simu ziorodheshwe kwenye soko la hisa DSE, yamekuwa na mafanikio hafifu hata kuhitajika kubadilisha sheria kwasababu sera mbovu za kiuchumi zimepunguza uwezo wa Watanzania kutumia fursa hizo kuwekeza. Ndio sababu majuzi kampuni ya Vodacom imejaribu kuongeza muda kwa IPO pamoja na sasa kuruhusu wasio wazawa kununua hisa hizo.

Mikopo ya benki kwa sekta muhimu

Sekta binafsi kama injini ya Uchumi inategemea zaidi mikopo kugharamia uwekezaji. Hata hivyo, takwimu za BoT kuhusu mwenendo wa mikopo kwa sekta binafsi kwa ulinganisho wa mwaka 2015 dhidi ya 2017, ni kielelezo tosha kwamba uchumi umevurugwa.

Ndani ya miaka miwili kiwango cha mikopo isiyolipika (Non Performing Loans – NPL) kilivuka wastani wa asilimia 5% na kufikia asilimia 8%. Benki kadhaa zilifungwa kutokana na tatizo la mikopo isiyolipika na zilizobaki kuyumba vibaya kutokana na mdodoro wa biashara uliosababisha ongezeko la mikopo isiyolipika.

Ni hali hii ilisiyosababisha wawekezaji na wafanyabiashara kuhofu kuchukua mikopo ya kibiashara kwa upande mmoja na benki nazo kuhofu kutoa mikopo kwa wafanyabiashara na hivyo kuongeza vikwazo vya upatikanaji mikopo kwa sekta binafsi kama njia ya kukabili tatizo la uwepo wa wimbi la mikopo isiyolipika kutokana na kuyumba kwa biashara.

Ununuzi na mauzo nje

Kwenye manunuzi nje (Imports) ni kwamba manunuzi ya bidhaa na huduma nje yalifikia dola za Marekani milioni 13,305.2 mwisho wa Mei 2015 ukilinganisha na manunuzi ya $9,738.8M, Mei 2017 sawa na tofauti ya $3,566.4 (sawa na Tsh 7,489.44bn.)

Mauzo jumla ya bidhaa na huduma nje ni kigezo muhimu katika kupima uchumi unaokuwa au kusinyaa. Kipindi cha Mei 2017, mauzo jumla yalikuwa $ 8,774.9M ukilinganisha na mauzo ya $9,454.5M kipindi kama hicho mwaka 2015. Hii ni sawa na tofauti ya $679.9M au Shilingi Trilioni 1.5.

Hivyo biashara ya nje kwa ujumla (import & export) imeanguka kwa takribani shilingi Trilioni 10. Hiki ndicho IMF imesisitiza kuwa uchumi wa Tanzania unapita katika kipindi wataalamu wa uchumi wanaita SOFT PATCH, yaani unachechemea.

Mwenendo huu unathibitisha msimamo wa taasisi ya ujasusi kiuchumi ya Economic Intelligence Unit kwenye ripoti yao kwa Tanzania Julai 2017 inayoonesha kwamba uchumi wa Tanzania unatarajiwa kuporomoka ukuaji wake na kufikia asilimia 5.2% ifikapo mwaka 2021.

Deni la Nje

Deni la nje kufikia Mei 2017 lilifikia $17,907.2M kutoka deni la $14,762.7M sawa na ongezeko la deni la nje kwa kiasi cha $3,144 au shilingi Billion 6,916bn kwa miaka miwili tu.

Na deni la ndani kufikia Mei 2017 lilifikia 11,353bn kutoka 7,707.3bn mwaka 2015 sawa na ongezeko la shilingi 3,645.7bn. Kwa ujumla kwa miaka miwili, kuanzia Mei 2015 mpaka Mei 2017, deni la taifa limeongezeka kwa zaidi ya shilingi 11,493bn. (Trilioni 11.5). Serikali imeendelea kudai kuwa deni ni himilivu. Badala ya kuelekeza nguvu na mikakati mikubwa kwenye uwekezaji, Serikali ya Magufuli inapambana na wawekezaji, wote wa nje na ndani.

Mahusiano baina ya sekta binafsi na Serikali yako shakani zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Investors Confidence inatoweka kwa kasi. Ni vigumu sana hata kwa wawekezaji wa ndani kuchukua   “Risk” kuwekeza katika nchi isiyoheshimu demokrasia, Katiba, Utawala wa Sheria, Kanuni, mikataba na hata utu.

Tunakimbiwa na tutakimbiwa zaidi, huku tukimpongeza “Bwana Mkubwa” kuwa anainyoosha nchi! Bila kuongeza uzalishaji, deni hili litaielemea serikali kama hadi sasa halijailemea.

Kwa sasa, tunatumia asilimia 80 ya makusanyo yote ya kodi kulipa mishahara na deni la taifa tu. Tunabakia na asilimia kama ishirini ya makusanyo kuendesha serikali na kutekeleza miradi ya maendeleo. Hali hii haikubaliki na ni muujiza kutoka kwenye umasikini.

Kwa ujumla mwendo wa uchumi (economic trend) wetu ni mbaya. Mauzo ya nje yameporomoka, manunuzi kutoka nje yameporomoka, mikopo sekta binafsi imeporomoka, deni la taifa linapaa kuliko kipindi chochote, biashara zinafungwa kuliko kipindi chochote, bado serikali inasema uchumi unakua.

Tunatoa wito kwa wachumi kufanya uchunguzi wa kina tusiingie kwenye mkumbo wa kupika takwimu za uchumi ili kupata umashuhuri wa kisiasa. Siku zote tukumbuke kuwa mficha ugonjwa, kifo humuumbua. Wananchi sasa wanaumizwa kihakika na hali ngumu ya maisha. Serikali inapashwa kuelewa hili na kuweka haraka mpango mkakati wa muda mfupi wa kurekebisha mserereko huu. Taifa halipaswi kubweteka. Aidha kupambana na ufisadi pekee hakuwezi kuwa tiba ya uchumi unaoporomoka.

Kwa miaka miwili ya Rais Magufuli ameangusha biashara yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 10.