MAMBO 14 KUHUSU MWL. JULIUS KAMBARAGE NYERERE!

Katika kumbukumbu ya kifo cha baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere, ni muhimu tukaendelea kumfahamu na kumkumbuka kwa kurejea historia yake kwa faida yetu kama watu ambao maisha yake yametugusa kwa namna moja au nyingine!

Chanzo cha mambo haya ni vitabu na maandiko ya watu mbalimbali mathalani yeye mwenyewe [Mwl. Nyerere], John Illife, Jack Nyamwaga, Erasto Mang’enya, Thomas Molony, James Irenge na Vedastus Kyaruzi. Wengine ni Andrew Kajungu Tibandebage, Pius Msekwa, Baba Mtakatifu Arthur Wille na wengine.

1) Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa April 13, 1922 katika kijiji cha Mwitongo Butiama. Tarehe yake ya kuzaliwa haikuwa inafahamika mpaka ‘Omugabhu’ (mtabiri) Mzee Mtokambali Bukiri alipoikumbuka wakati Nyerere akiwa chuoni Makerere.

2) ‘Mugendi’ ni jina ambalo wazazi wa Nyerere, Burito Nyerere na Mugaya Nyang’ombe walimpa baada ya kuzaliwa. Jina la Mugendi lilibadilishwa na mtabiri(umugabhu) baada ya kulia sana mfululizo, hivyo akapewa jina la Kambarage lenye maana ya mzimu (erisambwa). Baada ya zoezi hilo, kilio kiliisha na hali hiyo ikaambatana na mvua kubwa kama ishara ya baraka!

3) Mwalimu alipata Elimu yake ya msingi katika shule ya Mwisenge, baadae Tabora boys (The Eton of Tanganyika) kwa masomo ya Secondary. Mwalimu alijiunga na chuo kikuu cha Makerere kabla ya kujiunga na chuo kikuu cha Edinburgh mwaka 1949 kilichopo nchini Uingereza.

4) Inasemekana Chief Mohamed Makongoro wa Ikizu ndiye alimsihi Mzee Burito Nyerere kumpeleka Kambarage shuleni baada ya kugundua uwezo wake mkubwa wa akili. Hii ilichagizwa zaidi na umahiri wa Kambarage katika mchezo wa bao(usoro).

5) Baba wa Kambarage Mzee Burito Nyerere alikuwa chief wa pili wa Uzanaki baada ya chifu wa kwanza Buhoro kuondolewa kwenye nafasi hiyo na wakoloni. Kumekuwepo na sababu tofauti za chanzo cha kuondolewa kwake mathalani Thomas Molony anasema aliondolewa kwasababu ya kutojiamini na uoga kwa Wakoloni kupita kiasi lakini Kambarage aliwahi kunukuliwa akisema aliondolewa kwasababu ya ulevi.

6) Chanzo cha jina la “Wazanaki” inasemekana ni “waja na ki?” lenye maana “wamekuja na nini?. Swali hili liliulizwa na Wajita ambao ndio wenyeji wa eneo la Musoma baada ya wazanaki kufika eneo hilo kwa mara ya kwanza wakitafuta makazi.

7) Chief Burito ndiye muasisi wa utaratibu wa kutembeza mkanda uliofahamika kama Urukobha katika kuzunguka maeneo yote ya uzanaki na maeneo jirani kwajili ya kutibu maeneo hayo, kuondoa mikosi na majanga. Waandishi wengi wanahusisha urokobha na Mwenge wa uhuru unaotembezwa nchi nzima kila mwaka hivyo upo uwezekana kuwa Kambarage alirithi utamaduni huo kutoka kwa Baba yake.

8) Kambarage Nyerere alibatizwa December 23 na Father Aloysius Junker katika kanisa Katoliki ushirika wa Nyegina. Kwa kubatizwa kwake, aliweka rekodi ya kuwa mtu wa kwanza Butiama na Mzanaki wa kwanza kubatizwa. Alipewa jina la Julius. Hata hivyo, Nyerere anakiri kuwa Baba yake angekuwa hai, huenda asingefurahishwa na uamuzi huo wa kubatizwa.

9) Chief Burito Nyerere alimlipia mahali Magori Watiha akiwa na miaka mitatu kwajili ya kuolewa na Nyerere hapo baadae. Hii ni sehemu ya tamaduni za Wazanaki. Tofauti na matarajio ya wengi, Nyerere aliamua kumuoa Maria Magige aliyekutanishwa naye na Mwalimu Nestori Nyabambe na mke wake Anastanzia. Inasemekana mabadiliko haya yalisukumwa zaidi na sababu za kielimu na kiimani/dini(tofauti na Magori, Maria alikuwa Mkatoliki na Msomi wa ualimu). Kwa mujibu wa taratibu za Wazanaki, familia ya Magori walirejesha mahali (ng’ombe 10) kwajili ya Nyerere kumlipia Maria. Hata hivyo, mama wa Maria Bi Hannah Nyashabora alimtaka Julius Nyerere Kuongeza ng’ombe 2 kwakuwa Maria alikuwa binti Msomi. Pamoja na kwamba Nyerere hakuwa na uwezo huo(alikuwa ametoka masomoni Edinburgh) Nyerere alilazimika kukopa kutoka kwa rafiki yake William Collins ili afanikishe utaratibu huo.

10) Sera ya Ujamaa inahushwa na makuzi ya Nyerere ya utamaduni wa Kizanaki unaofahamika kama “iriisaga” wa watu kufanya kazi pamoja na kugawana mali kwa usawa. Hata hivyo wengine wanaamini pamoja na vitabu vingi vya watu mbalimbali alivyosoma na kufundishwa na waalimu wake, sehemu kubwa ya sera ya ujamaa ilitokana na kitabu cha Mwandishi wa kichina Tung Fei kinachoitwa “The Village of Kaihsienking in the Yangtze Valley” ambacho kijiji hicho (Kaihsieniking) sio tu kwamba nchi yake ni sawa na Tanganyika, lakini pia kina ufanano na sera ya vijiji/Ujamaa ambayo baadae mwalimu aliiasisi nchini. Mfano mwingine wa ufanano huo ni mfumo wa nyumba kumi (ten-house cell system) ambao Mwandishi Fei aliuweka kwenye kitabu hicho. Kitabu hiki ni Kitabu alichoelekezwa kusoma na Mwalimu wake Prof Richard Pares wa Edinburgh.

11) Kwa mujibu wa Father Arthur Wille wa Edinburgh, Mwalimu Nyerere akiwa Edinburgh, alimwandikia barua rafiki yake ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa St. Mary’s na mshauri wake, Father Richard Walsh kuwa anafikiria kumtumikia Mungu kwa njia ya uongozi wa Kiroho. Jibu la Father Walsh lilikuwa kinyume na matarajio ya Nyerere kwani alimwambia anaona anaweza kufanya mengi mazuri kwajili ya watu kwa kuwa Kiongozi wa kisiasa.

12) July 10, 1943 Nyerere akiwa mwaka wa kwanza Makerere, aliandika makala kwenye gazeti la “Tanganyika Standard” iliyoitwa “African Socialism” akikosoa vikali mfumo wa Kibepari aliouita wa kinyonyaji kwa waafrika. Nyerere alitumia jina la JUKANYE kwenye makala hiyo kali kama ufupisho wa majina yake matatu. Kwa mujibu wa mwandishi Ruth Schachter Morgenthau, anahusisha makala hiyo yenye dhana ya “ujamaa wa Kiafrika” (African Socialism) na ile iliyosisiwa mwaka 1940 na wanaharakati wa Senegal Leopold Sedar Senghor na Mamadou Dia ambao walikuwa viongozi wa tawi la chama cha kifaransa “Francaise de I’internationale Ouvriere” nchini humo!

13) Mwalimu Nyerere akiwa masomni Edinburgh, Agost 20, 1950 aliandika Makala nyingine ikielezea mstakabali wa Afrika Mashariki, mifumo ya ubaguzi wa rangi na ukembe wa kisiasa [Future of East Africa: Racial Antagonism and Political immaturity]. Katika makala hiyo, pamoja na mambo mengine, Nyerere alisisitiza usawa kwa kila binadamu.

14) Mwalimu Nyerere akiwa Chuoni Makerere mwaka 1944 alifanikiwa kuwashawishi wanafunzi wenzake wa Kitanzania; Hamza Mwapachu, Vedastus Kyaruzi, Andrew Tibandebage, David Makwaia(kipenzi cha Governor Sir Edward Twining) na Abdulah Fundikira kuunda umoja Wa wanafunzi wa Tanganyika (TSA) ambao baadae walirudi chini kuhuisha harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika.

Happy Nyerere Day

_____________
Bob Wangwe