MAKOSA NA USAHIHI WA ZITTO KABWE, TUNDU LISSU.

Kukosoa ni jambo jepesi lakini lenye uzani mkubwa kwa kulitazama kwa vipimo sahihi. Ukosoaji kimantiki hujengwa na matawi mawili, inategemea mkosoaji anashika tawi lipi.

Kwa bahati mbaya watu wengi hushika tawi jepesi. Mbaya zaidi ni kuwa hufikia hata viongozi wakubwa nao kushika tawi hilo katika ujenzi wa hoja zao.

Katika ukosoaji; tawi la kwanza ni kuponda. Hili ndilo ambalo wengi wanalikumbatia, maana halisumbui ubongo. Ni kukosoa tu. Tawi la pili ni falsafa. Hapo ndipo pazito.

Ni kwa kutambua thamani ya ukosoaji unaojengwa na falsafa, ndiyo maana tuzo za Uandishi wa Habari zenye heshima kubwa Marekani, Pulitzer Prize, kuanzia mwaka 1970, ilianza kutolewa tuzo ya Ukosoaji Uliotukuka (Pulitzer Prize for Criticism) kila mwaka.

Mshindi wa kila mwaka huzawadiwa medali ya dhahabu na fedha, dola 15,000, sawa na karibu Sh34 milioni za Tanzania. Hiyo ni kuonesha kuwa ukosoaji wenye kujengwa na falsafa si kitu chepesi, kwani msingi wake ni tafakuri ya kina.

Kuna maneno mawili ya Kiingereza, Critic (lenye asili ya Kigiriki) na Critique (lenye asili ya Kifaransa), hayo ndiyo matawi mawili ya ukosoaji. Critic ni kuponda au kuhukumu, Critique ni falsafa.

Critic ni kuielekea hasi na kuisema bila mzani. Unakosoa tu. Critique ni falsafa ambayo hujengwa na mzani wenye kuimulika chanya na kuiweka dhahiri hata kama ilikuwa imejificha, kisha kuigusa hasi kwa namna ya kuifafanua ili iwe chanya.

Ndani ya Critique ndipo kwenye ukosoaji wenye kujenga (constructive criticism) na ufikiri wa kina (critical thinking). Mkosoaji anayetumia tawi hili huwa hashambulii, bali hujenga hoja zenye kumfanya hata anayekosolewa kujifunza.

ZITTO NA LISSU

Hivi karibuni uliibuka mzozo mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, ukianzia kwenye Twitter, baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, kuandika ujumbe wa kumkosoa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.

Zitto alimkosoa Lissu kuhusu hoja yake ya kutaka Jumuiya za Kimataifa na nchi wahisani kuinyima Tanzania misaada kwa sababu Serikali haifuati misingi ya demokrasia na utawala bora.

Lissu katika hoja yake, alizungumzia mambo mengi, akitoa na mifano kadha wa kadha kuonesha jinsi demokrasia nchini inavyominywa na namna nguzo za utawala bora zinavyovunjwa.

Zitto katika ukosoaji wake, hakugusa maeneo mengine ambayo Lissu aliyazungumzia kufikia hitimisho la kutaka nchi inyimwe misaada, yeye alikwenda moja kwa moja kwenye hitimisho.

Zaidi, Zitto kwa namna alivyoandika, inaonekana alikerwa na kauli ya Lissu ya kutaka nchi inyimwe misaada. Na kwa kukerwa huko alitumia lugha kali dhidi ya Lissu.

Je, kwa lugha kali ambayo Zitto alitumia, ndiyo kusema alikosea? Jawabu ni hapana. Zitto alikuwa na hoja ya msingi lakini aliamua kutumia tawi jepesi kwenye ukosoaji, matokeo yake alieleweka vibaya na kusabibisha ashambuliwe na watu hususana wana-Chadema.

Usahihi wa Zitto upo kwenye makosa ya Lissu; kweli nchi inyimwe misaada? Tanzania ambayo ni tegemezi kwa sehemu kubwa, ikinyimwa misaada watakaoathirika ni akina nani?

Tanzania ambayo kwa sehemu kubwa bajeti iliyopita (2016-2017), ilishindwa kutekelezwa, sababu ikiwa kusuasua kwa wahisani katika uchangiaji wa bajeti, je, nchi ikinyimwa kabisa misaada itakuwa mgeni wa nani?

Ni kweli kuwa nchi ikinyimwa misaada, Serikali itashindwa kutimiza malengo yake. Hata hivyo, malengo yote ya Serikali yapo kwenye msingi wa kuwahudumia wananchi. Hivyo, nchi ikikosa misaada wananchi watakosa huduma stahiki kutoka serikalini.

Kiongozi wa Serikali ni Rais John Magufuli ambaye kwa nafasi yake, anao mkataba wa kuhudumiwa na Watanzania kila kitu kisha naye ndiyo aiongoze Serikali yake kuwapa Watanzania huduma bora.

Kwa mantiki hiyo ni kuwa nchi ikinyimwa misaada, Serikali itapungukiwa uwezo wa kuwahudumia wananchi. Wakati huohuo, Watanzania wataendelea kubeba mzigo wa kumhudumia Rais wao (Dk Magufuli).

Kumbe sasa ukweli upo dhahiri kwamba nchi ikinyimwa misaada, mwathirika mkuu ni Taifa zima. Wakati huohuo, Watanzania hawatakwepa kumhudumia Rais wao. Mpaka hapo, nani ataathirika zaidi nchi ikinyimwa misaada?

Hivyo basi, Lissu anaweza kuwa na hoja ya msingi kwenye ukosoaji wake kwa Serikali ya Rais Magufuli kwa namna inavyowahudumia Watanzania, hasa eneo la demokrasia na utawala bora, lakini hakuwa sahihi kwenye ombi la nchi kunyimwa misaada.

Zitto alikuwa sahihi kumpinga Lissu kwa sababu misaada si kwa ajili ya Rais Magufuli, bali kwa Watanzania. Nchi ikinyimwa misaada hakomolewi Rais Magufuli, isipokuwa Wananchi ndiyo watakiona cha moto.

MAKOSA YA ZITTO

Makosa ya Zitto yanaundwa na jukwaa alilochagua kutumia. Twitter si mtandao ambao unampa mtumiaji nafasi pana ya kuandika. Ni jukwaa finyu katika maandishi.

Lissu yeye alizungumza na vyombo vya habari, hivyo hoja zake alizipanga kwa upana. Zitto yeye hakuwa na fursa pana ya kuchambua hoja yake ya kumpinga Lissu, kwani alitumia Twitter yenye ufinyu wa nafasi kimaandishi.

Ni kwa sababu ya ufinyu wa nafasi, Zitto hakutumia Critique (falsafa), bali aliegemea kwenye Critic (kuponda). Kiongozi anapaswa kujenga ukosoaji kifalsafa ili aeleweke vizuri bila kushambulia.

Mtaalam wa saikolojia ya ukosoaji, raia wa Japan, Mai Kagawa, anaeleza kuwa ili ukosoaji wa kifalsafa (Critique), ufike vizuri, inabidi ushauri uwe katika muundo wa mkate wa sandwich au burger.

Ni kwamba sandwich na burger mikate yake hukatwa katikati, halafu ile sehemu ya kati hujazwa nyama au samaki, vilevile mbogamboga, kachumbari kulingana na matakwa.

Mai anasema kuwa ile sehemu ya kati yenye kujazwa nyama au samaki na kachumbari, ndiyo ukosoaji wenyewe, halafu mkate wa juu ni pongezi panapostahili na chini ni ainisho la makosa.

Tafsiri ni kuwa ukosoaji wa falsafa hujengwa na pongezi au kukubali palipo na usahihi kisha kuainisha upungufu au makosa, mwisho unajaza ushauri katikati ya pongezi na ukosoaji.

Mathalan, yapo mambo mengi ambayo Zitto amekuwa akiyalalamikia na ni hayohayo ambayo Lissu aliyazungumzia. Zitto alipaswa kukubaliana na Lissu katika hayo ndipo ampinge kwenye eneo la nchi kunyimwa misaada.

Hakuna jambo jipya ambalo Lissu alililalamikia ambalo Zitto hajawahi kulalamika kuhusu demokrasia na utawala bora. Ni Zitto aliyewahi kutamka kuwa Rais Magufuli anapaswa kuwa Rais wa muhula mmoja (miaka mitano) kwa sababu anaminya demokrasia na hafuati utawala bora.

Uchambuzi wa Lissu uliegemea hapo kwenye maeneo hayo mawili; demokrasia na utawala bora. Hivyo, Zitto hapaswi kuonekana anapingana na Lissu, bali anapaswa kuonekana anapingana na tamko la nchi kunyimwa misaada.

Hata hivyo, kufikia kuonekana anakubaliana na Lissu lakini anapingana na suala la nchi kunyimwa misaada, Zitto alitakiwa autoe ushauri wake kwa mtindo wa sandwich. Kwamba juu angekubali, chini angekosoa, katikati angejaza ushauri.

Zitto alisema Tanzania ni nchi huru, kwa hiyo demokrasia ipiganiwe ndani. Ni kwamba Zitto hapingi kuwa demokrasia ina walakini, lakini anasema inaweza kupiganiwa ndani. Inapiganiwaje ndani? Zitto alipaswa kujenga hoja mahsusi ili aeleweke barabara.

SOMO LA JUMLA

Kama Zitto angeandika makala yenye kuchambua ukosoaji wake kwa hoja za Lissu, pengine siyo tu angeonekana hampingi Lissu, bali pia angesaidia watu wengi kuelewa madhara ya nchi kunyimwa misaada, vilevile namna bora ya kuipigania demokrasia ndani ya nchi, pasipo kutoka nje.

Na kwa vile ufinyu wa nafasi umekuwa chanzo kikuu. Ni somo kubwa kwa viongozi kujiepusha na ukosoaji wa hotuba kwa Twitter, maana hukosa uwanja mpana wa kufafanua hoja.

Kingine ni kujiepusha na hisia wakati wa kukosoa. Hata kwenye Twitter, hali isingekuwa mbaya kama Zitto angeandika: “Pamoja na kukubaliana na Lissu kwa aliyosema kuhusu demokrasia, sikubaliani naye kwenye suala la nchi kunyimwa misaada. Watakaoumia ni Watanzania na siyo Rais Magufuli.”

Lissu pia katika ushauri wake, awe anajiepusha na mashambulizi. Ujenzi mzuri wa hoja hustawishwa na uchambuzi wa tatizo na kuelimisha. Suala la demokrasia linamhusu kila Mtanzania, wakiwemo wana-CCM wasioambiwa kitu juu ya Rais Magufuli, liwake jua, inyeshe mvua.

Hata hivyo, haohao wasioambiwa kitu kwa Rais Magufuli, iwe kwa usahihi au makosa, pengine wanaweza kumuunga mkono Lissu kama watasikia hoja yenye ukosoaji wa staha na wenye kuelimisha.

Ikiwa lugha yenye kutumika siyo nzuri, hapohapo hupoteza mantiki na kujaa ukakasi kwa wale wasiopenda kusikia Rais Magufuli anakosolewa. Matokeo yake ni kusababisha elimu isipenye kwa wengi.

Lissu anapaswa kufahamu kuwa kumkosoa mtu kwa lugha ya kuudhi haimaanishi ndiyo ujumbe unafika barabara, isipokuwa huchochea shari. Anayekosolewa hukosa nafasi ya kujitathmini na kujirekebisha, bali hukasirika na kuona kafedheheshwa.

Hili pia kwa Zitto, lugha aliyotumia kumkosoa Lissu kuhusu ombi lake la nchi kunyimwa misaada na wahisani haikuwa nzuri. Ilikuwa na ukakasi mwingi.

Wapo wana-Chadema wangeweza kuelimika na kumuunga mkono Zitto, lakini lugha aliyotumia haikuwa njema kwa kiongozi wao wanayempenda na kumwamini, matokeo yake wana-Chadema wamekuwa na kasi kubwa ya kujibu mashambulizi kwa Zitto.

Ushauri wa jumla kwa wanasiasa ni kuwa na matumizi bora ya lugha zenye kusikilizika. Watumie maneno yenye kuelimisha. Maneno yanayotamkwa baada ya tafakuri. Maneno yaliyo na nakshi za kifalsafa.

Ndimi Luqman MALOTO