KIONGOZI MWINGINE WA CHADEMA AMVAA MBOWE, ASEMA MAGUFULI NI ZAIDI YA NYERERE

Ndugu Watanzania wenzangu husasan Wana CHADEMA wote,

 

Mimi Benson Mramba (32) ambaye nimekuwa Mfuasi na Mwanachama muaminifu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) tangu mwaka 2005 na kufanikiwa kutumika kama kiongozi katika ngazi mbalimbali za chama kama ifuatavyo:-

I. 2005-2008 Mwanachama wa kujitolea (Volunteer) katika Kurugenzi ya Vijana na Mambo ya nje Makao Makuu ya Chama wakati huo ambapo Mimi pamoja na wenzangu Mh.John Mnyika (Aliyekuwa Mkurugenzi wetu), David Kafulila na wengine tulikuwa na majukumu ya kuratibu shughuli za vijana hususan wanafunzi wa Vyuo Vikuu.

II. 2008-2009 Katibu wa CHADEMA Kata ya Kibamba Manispaa ya Ubungo wakati huo Kinondoni Jijini Dar es Salaam.

III. 2009-2013 Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Tanga.

IV. 2011-2014 Afisa Mwandamizi Makao Makuu ya Chama niliyekuwa nashughulikia mambo ya TEHAMA (Information Technology Officer ).

V. 2014-2016 Afisa Mwandamizi Makao Makuu niliyekuwa nashughulikia Mambo ya Utawala, TEHAMA na Usimamizi wa Rasilimali za Chama (Administration, ICT, and Resources Management Officer)

Nimeamua kwa hiari yangu na dhati ya moyo wangu kufuata falsafa ya Dr Azaveli Lwaitama ya miaka mingi, ambapo yeye baada ya kuona mambo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yalikuwa hayaendi kwa kufuata misingi ya kuanzishwa kwake aliamua kuwa Mwanachama mfu wa Chama cha Mapinduzi kwa miaka mingi. Katika kipindi chote hicho tangu nilipomfahamu alikuwa akikikosoa Chama chake na Viongozi wake na kuwaunga mkono hadharani watu wote na Taasis waliokuwa wakisimamia na kupigania misingi ile ambayo iliachwa na Chama Cha Mapinduzi kwa muda mrefu.

 

Hivyo basi kuanzia tarehe hii ya leo 14/06/2017 Mimi Benson Mramba nimeamua kuwa Mwanachama Mfu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kwa sababu kuu mbili:-

 

1. NINAMUUNGA MKONO RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Mh. John Pombe Magufuli ambaye kwa sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa ni kiongozi wa mvuto kwangu (Role Modal) tangu nilipoanza kujihusisha na siasa wakati huo yeye akiwa ni Waziri katika Serikali za CCM. Tangu amechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesimamia na kutekeleza mambo mengi ambayo nimekuwa nikiyapigania kama Mwanachama wa CHADEMA kwa muda wote wa miaka zaidi ya 10 ya uanachama wangu. Hivyo kwa muda mrefu nimekuwa nikimpongeza kimya kimya nafikiri ni wakati mwafaka sasa nipate fursa ya kuungana na Watanzania wenzangu wengi kumpongeza na kumuunga mkono hadharani na kwa uhuru zaidi.

 

 

2. NINAMPINGA MWENYEKITI WA CHADEMA FREEMAN MBOWE NA GENGE LAKE KUENDELEA KUWA NA UHALALI WA KUKIONGOZA CHAMA

Kwa miaka mingi nimekuwa siridhishwi na uongozi wa Mwenyekiti wangu na wapambewake. Nimekuwa nikimpinga kwa siri kutokana na nafasi za uongozi nilizokuwa nazo. Aidha niliiamini kwa kiasi fulani Kamati Kuu ya Chama na Sekretarieti yake wakati wa Katibu Mkuu Dr. Wilbrod Slaa na upinzani wa ndani uliokuwepo wakati wa akina Zitto Kabwe , Kitila Mkumbo na Wajumbe wengine makini wa Kamati Kuu ya Chama waliokuwa na ujasiri wa kumkosoa na kumsema Mwenyekiti wetu bila woga tofauti na sasa.

 

Kuanzia leo nimeamua kuanza kumpinga hadharani Mwenyekiti wangu kwa sababu kuu mbili ambazo zimetuumiza WanaCHADEMA kwa muda mrefu sana mpaka leo:-

I. Matumizi Mabaya sana ya Madaraka Hususan katika maswala ya Uteuzi na Uchaguzi ndani ya Chama pamoja na ukosefu wa Maadili ya Uongozi. Matumizi mabaya kabisa ya Madaraka kuwahi kutokea ndani ya Chama ni Uteuzi wa Wagombea nafasi za Ubunge wa Majimbo na Wabunge wa Viti Maalum 2015 wa Chama chetu pamoja na Uchaguzi wa Viongozi wa Chama ngazi ya Taifa 2014 na Kanda 2017

II. Matumizi Mabaya ya Mali za Chama na Fedha za Ruzuku. Katika hili ninamuomba Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mh. John Pombe Magufuli ambaye siku zote amekuwa akisema yeye ni Rais wa Watanzania wote bila kujali vyama aagize uchunguzi wa kiserikali kama Taasis ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na CAG ili kumdhibiti Mwenyekiti wetu na mtandao wake dhidi ya matumizi mabaya na ufisadi wa fedha ambazo Wanachadema wote tumezipigania kwa Jasho na Damu za wenzetu. Aidha tuhuma hizi ni za kila uchaguzi ila kwa sababu hakuna wa kumgusa ameendelea nazo.

Mwenyekiti Mbowe amekuwa na kawaida ya kukidai Chama fedha kila baada ya Uchaguzi mkuu kwa madai kuwa amekikopesha Chama. Mikopo hiyo huwa haina ushahidi wowote lakini hujilipa na wanaojaribu kuhoji huandamwa na genge lake ikiwa ni pamoja na kuitwa wasaliti na kufukuzwa uanachama au kuvuliwa uongozi. Baada ya Uchaguzi wa mwaka juzi 2015 pamoja na ujio wa Lowassa na Marafiki zake wenye fedha na misaada mingi toka vyama marafiki na wapenda mabadiliko wengi bado Mwenyekiti wetu ameleta madai ya Tsh Bilioni 7 kwa Chama fedha ambazo ameanza kujilipa kinyume cha utaratibu na kukiacha Chama taabani kifedha hali ya kuwa tunapata ruzuku ya zaidi ya Tsh Mil 300 kwa mwezi kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

 

Kwa uamuzi wangu huu wa leo ninaamini nitakuwa huru kuendelea kutetea maslahi ya nchi yangu Tanzania na kuimarisha demokrasia nchini kwa uhuru zaidi bila unafiki kutetea damu za WanaCHADEMA waliodhulumiwa haki zao na utawala wa Mwenyekiti wetu na wale waliokubali kutoa maisha yao kwa ajili yaChama chetu.

 

Ni matumaini yangu kuwa nitakuwa msemaji wa Wanachama na Viongozi wangu wa CHADEMA popote nchini pale ambapo mifumo ya ndani ya Chama inawaminya kusema mambo yanayowakwaza. Aidha nitaweza kumshauri Rais na kushirikiana nae katikakuijenga Tanzania mpya ya uchumi wa Kati kwa kupiga vita ufisadi wa aina zote hata ulio ndani ya vyama vya siasa kwani nazo ni fedha zaWananchi wa Tanzania.

 

Imetolewa leo tarehe 14.06.2017 Tanga.

 

Benson Mramba

Mwanachama Mfu wa CHADEMA.