HUYU NDO THOMAS SANKARA RAIS MASKINI KULIKO WOTE KUWAHI KUTOKEA BARANI AFRIKA, MWENYE UZALENDO WA KUSHANGAZA.

Mnamo august 1983, vijana wawili, makapteni wa jeshi na wanamapinduzi, Thomas Sankara na Blasius Compaore, waliipindua serikali ya Rais wa wakati huo katika nchi iliyokuwa ikijulikana kama Upper volta, rais huyu aliitwa Baptiste Ouedraogo.

Vijana hawa wakiwa katika fikra za Karl Max, wakiwa na ndoto nyingi za kuijenga Upper volta, walibadili kabisa historia ya taifa hilo, walibadili jina la nchi na kuitwa Burkina faso, maanake nchi ya watu, country of honorable citizen.

Uchapakazi wa vijana hawa (Sankara na Compaore), Thomas sankara akiwa ndiye rais unaweza kufananishwa na ule wa Fider Castrol na Che Guavera, kabla haujachuja kule Cuba..

Haiyumkini Sankara alikuwa anatumia baiskeli kutembelea vijijini kuhimiza maendeleo, wakati pacha wake (Compaore) wakiwa kama pete na kidole.

Urafiki wa makapteni hawa wa jeshi la Burkinabe, ulikuwa mkubwa kiasi ambacho, wakati wanausalama walipomwambia Sankara kuwa Compaore ana mpango wa kumpindua na kumuua, yeye aliwajibu kuwa compaore asingeweza kufanya hivyo, labda mtu mwingine.

Blaise Compaore alikutana na Thomas Sankara mwaka 1976 katika mafunzo ya kijeshi Morocco na hapo walianza urafiki wao uliokuwa wazi kwa karibu watu wote waliokuwa wakiwafahamu nchini Burkina Fasso na nchi jirani.

Thomas Sankara alikuwa akiwaeleza wanausalama wake kuwa, hata kama Compaore angetaka kufanya hayo, hakuna wa kumzuia.

Ni wazi kuwa Kapteni Thomas Isidore Sankara alikuwa karibu sana na Blaise Compaore, kwa kiasi ambacho Blaise Compaore alikuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya Sankara.

kama ilivyotabiriwa na watu wengi wa karibu wa Thomas Sankara, Blaise Compaore aliongoza mapinduzi yaliyosababisha kifo cha Sankara mnamo mwaka 1987, na yeye mwenyewe (Compaore), huku akishuhudia rafiki yake kipenzi Sankara akiuwa, Akawa ndiye mrithi wa kiti cha Urais wa iliyokuwa Upper Volta baadaye Burkina Fasso.

Thomas Isidore Noël Sankara ni nani??

Isidore Noël Thomas Sankara alizaliwa tarehe 12.12.1949 Mjini YOKO katika nchi iliyokuwa ikiitwa Upper Volta (Volta ya juu) na kuuawa tarehe 15.10.1987 na wanajeshi wenzake wakiongozwa na rafiki yake Rais Blaise Compaore katika mapigano ya usaliti yaliyotokea Mjini Ouagadougou akiwa katika kikao cha utendaji wa kazi.

Thomas Sankara alipanda ngazi za kijeshi hadi cheo cha kaptenu pamoja na mwanajeshi Rafiki yake Blaise Compaore ANAYEJUA SIRI YA KIFO CHA CHA THOMAS SANKARA .

Kuna nyakati ambazo Blaise Compaore alipata kunena kwa kinywa chake katika shirika la kutetea haki za Binadamu duniani kwamba “kifo cha Thomasi Sankara kilikuwa ni ajali tu.

Mwaka 1981 Thomas Sankara alikuwa waziri wa mambo ya ndani katika serikali ya kijeshi ya Rais wa wakati huo wa Burkinabe ya zanani (Upper Volta) Jean Baptiste Major. Dr. na baadaye aliteuliwa kuwa waziri mkuu kwa kipindi cha kuanzia Mwezi Januari 1983 mpaka mwezi Mei alipokamatwa na kutiwa mbaroni na serikali ya Rais Major Jean Baptiste Dr kutokana na msimamo wake juu ya ukombozi kwa watu wote wa Volta ya Juu na kupendelea Marxist Revolution theories.

Thomas Isidore Noël Sankara alikuwa Rais wa Upper Volta (Volta ya Juu) kuanzia mwezi Agosti 4 1983 hadi mwezi Octoba 15 1987 baada ya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Major Dr Jean Baptiste yakiongozwa na Blaise Compaore na kuwa Rais wa TANO wa VOLTA YA JUU au BURKINA FASO baada ya kubadilishwa jina na Sankara.

Thomas Sankara aliyejulikana kama Che – Guevara wa Afrika alianzisha Program mbalimbali za kijamii na kiuchumi kuleta mabadiliko katika nchi za Afrika. Alibadilisha Upper Volta na kuwa Burkina Faso (land of Upright Men).

Alianzisha kampeni ya kuboresha Elimu na kutanua
Huduma za Afya kwa watu wa Burkina Faso maeneo ya vijijini hasa kwa watoto walio athirika na magonjwa ya Uti wa mgongo , Homa ya manjano, na surua.. na watoto karibu milioni 3 walipata tiba hizo..

Pia alianzisha kampeni ya upandaji wa miti kitaifa, na takribani miti Milioni kumi ilipandwa nchi nzima..

Pia alianzisha kampeni ya usafi nchini kote, kila mwananchi alipaswa kufanya usafi eneo alipo na Sankara mwenyewe alikuwa anashika fagio na kuingia barabarani kufanya usafi. Hiyo ni kampeni iliyoitwa mfagio wa mwananchi (le balai citoyen).

Aliongeza idadi ya wanawake katika serikali yake, ikiwa ni kampeni yake nchi nzima kupinga tohara kwa wanawake, pia alianzisha kampeni na baadae utaratibu wa kisheria wa kuwataka wasichana waliopata mimba wakiwa mashuleni kuendelea na masomo pia akaajiri wanawake jeshini, akawapa ajira katika sekta za umma ili kupunguza unyanyasaji wa kijinsia na kuleta uwiano na usawa nchini Burkina Fasso.

Pia ndoa za wasichana wadogo na za kulazimishwa haswa za kimila katika maeneo mengi ya Burkina Fasso zikapigwa marufuku.

Thomas Sankara ambaye hakutaka makuu kabisa na wananchi wa Burkina Fasso. Akiwa kama Rais wa nchi, alivaa nguo zilizotengenezwa Burkina Faso badala ya suti kutoka Paris na London. mara nyingi alionekana akiwa kwenye gwanda la jeshi.

Pia Thomas Sankara alifuta matumizi ya magari ya kifahari kwa viongozi na watumishi wote wa umma, yeye kama Rais alikuwa akitumia baiskeli au miguu kwenda kwa wananchi vijijini kuhimiza na kusimamia shughuli za kimaendeleo.

Alijikita sana kwenye kusimamia na kukuza sekta ya afya katika Burkinabe, alihimiza watu kujihusisha na kilimo akiwapelekea zana za kilimo na pembejeo bure kwa watu wa vijijini na kugawa ardhi kwa wananchi ili wajihusishe na kilimo.

Kwa muda mfupi sana akiwa kama Rais wa Burikna Fasso, aliweza kuifanya nchi hiyo kuagiza chakula kutoka nchi za nje na kuifanya nchi hiyo kuanza kuuza vyakula vyake nje akaanza kuifanya Burkina Fasso kuwa imara kiuchumi.

Sankara aliwahimiza watawala wa Afrika waache kuwaibia wananchi, waache kutegemea sadaka kutoka nje.

Sankara akawaambia madeni ya Afrika hayana uhalali kwa vile yalitokana na mikataba mibovu. Ndio maana hakuna maendeleo yaliyotokana na mikopo ya kigeni. Sankara akataka Afrika iache kulipa madeni yasiyolipika.

Mwalimu Nyerere naye wakati huo alisema mtu hawezi kulipa madeni wakati watoto wanakufa njaa.

Thomas Sankara alisema ukitaka kujua maana ya ubeberu angalia sahani yako ya chakula, utaona kila aina ya chakula unachokula kinatoka nje. Ndipo akahimiza Afrika ijitegemee kwa chakula, akisema: “Anayekulisha anakutawala”

Thomas Isidoré Nöel Sankara ni wazi aliwakasirisha sana mabeberu wa kimagharibi, hasa ubeberu wa Kifaransa uliokuwa ukitawala kupitia vibaraka wake wa Afrika kama Rais Felix Houphouet- Boigny wa Ivory Coast.

Chini ya uongozi wake (Thomas Sankara), Burkina Faso ililima chakula chake badala ya kuagiza kutoka nje.

Kwa hatua hiyo, Thomas Sankara akawa amewaudhi wakubwa wa dunia (mabeberu) kwa kukataa kwake mipango ya kurekebisha uchumi ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) huku hoja kubwa ya sankara ikiwa ni kwamba, mipango hiyo ni ya kinyonyaji.

Thomas Sankara aligawa ardhi kwa wakulima wadogo baada ya kuchukua kutoka kwa wawekezaji wa nje ambao walikuwa wameipora baada ya kupewa na uongozi uliopita.

Katika huduma za jamii alileta mabadiliko makubwa katika huduma za elimu, afya, maji na kuboresha miundombinu ya barabara kuunganisha sehemu mbalimbali za nchi hiyo.

Sankara katika kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinahudumia wanachi wa kawaida, Sankara alipambana na rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma, huku akimtaka kila mwananchi kujituma kulijenga taifa.

Thomas Sankara alikuwa mtu anayechukia rushwa na ufisadi, uvivu, uzembe, dhuluma na unyonyaji wa wananchi na rasilimali zao. Alitaka kuona watu wake wakifaidika kwa rasilimali za nchi yake.

Huyu ndiye Thomas Sankara ambaye alipunguza mshahara wake hadi dola 450 kwa mwezi, ambaye alitembea kwa baskeli katika mitaa ya Ouagadougu bila ya kulindwa. Alipoulizwa kwanini hana walinzi alisema wananchi ndio walinzi wake, hivyo hahitaji kuambatana na wanajeshi wenye bunduki.

Washauri wake mara kwa mara walimshawishi aachane na matumizi ya baisikeli.

Akaamua kutumia gari lenye bei ya chini (Renault 5) badala ya msururu wa mashangingi kama tuonavyo leo katika Afrika…

Hata hivyo alibaki na baiskeli yake mpaka alipokutwa na mauti, na akaunti yake ya benki ilikutwa na akiba ya dola 400 ambayo ni sawa na Tsh 850, 550/= (laki nane elfu hamsini na tano namia tano hamsini), kwa sasa, badala ya mabilioni mengi kama wanayoficha huko Uswisi watawala wetu leo.

Kumbuka, Thomas Sankara amedumu kwenye uongozi kwa kipindi cha miaka 4 pekee kabla ya mapinduzi yaliyoongozwa na Rafiki yake kipenzi. Blaise Compaore ambaye aliondoka na uhai wake, lakini kwa kipindi hiko cha miaka 4 akihudumu kama Rais, alitengeneza mageuzi makubwa sana.

Ndoto kubwa ya kila siku ya Thomas Sankara, ilikuwa ni kuifanya Burkinafasso kuwa moja kati ya mataifa makubwa Afrika kiuchumi.

Thomas Sankara alikataa hata picha yake (yeye kama Rais) kutundikwa katika majengo, na taasisi za serikali alisema hataki kutukuzwa.

Sankara alikuwa akipokea mshahara wa dola 450 kwa mwezi, mshahara mdogo kuliko viongozi wote barani Afrika kwa wakati huo.

Huyu ndiye Thomas Isidore Noël Sankara anayejulikana kama Ernesto Che Guevara wa bara la Afrika (alikuwa akivaa mavazi kama Che Guevara, mwenendo, matendo na malengo yake yalifanana na Ernesto Che Guevara, pia walikuwa marafiki wakubwa), aliyeiongoza nchi kwa muda wa miaka minne kabla ya kuuliwa na maadui wa mapinduzi wakiongozwa na kapteni Blaise Compaoré Aliuliwa nyakati za usiku na mara moja akazikwa kwa haraka. Ernesto Che Guevara naye alikuwa mwanamapinduzi wa Marekani Kusini aliyeuliwa na majasusi wa Marekani (CIA) na kisha kuzikwa kisirisiri.

Thomas Sankara aliyekuwa muumini wa fikra za kupigania Umoja wa Afrika au Pan Africanist mara nyingi alionekana kutopendwa na mataifa ya magharibi kutokana na fikra zake za kupinga dhuluma za wakoloni kunyonya watu wanyonge.

Mwaka 1985, Thomas Sankara alikaririwa akisema kuhusu falsafa yake kisiasa iliyokuwa maarufu, ilikuwa ikisema;

‘you cannot carry out fundamental change without a certain amount of madness’, yaani kwa tafsiri isiyo rasmi, hauwezi kuleta mageuzi ya msingi bila kuwa na kiasi fulani cha ukichaa ndiyo maana mabeberu walieneza propaganda kwamba Sankara ni kichaa anayeingoza Burkina Fasso.

Pamoja na yote na mengi mazuri, wapinzani ndani na nje ya nchi ya Burkinafasso, walisikika wakimlaumu Sankara kwa kupiga marufuku vyama huru vya wafanyakazi na vyama vya siasa.

Pia Sankara alianzisha Mahakama za wananchi ‘people’s revoluntionary tribunals’ ambazo zililenga kutoa hukumu kwa wapinga mapinduzi, wafanyakazi wazembe Jambo ambalo lilileta hamasa ya watumishi wa umma kufanya kazi kwa nguvu wakiogopa hukumu.

Ila hatua hiyo ilipigwa vita saba na wapinzani wake. Kumbukumbu kubwa ya wananchi wa Burkinabe (Burkina fasso), kuhusu Kapteni Thomas Sankara, ilikuwa ni wiki moja kabla ya kuuwawa kwake alitabiri, na alikaririwa akisema:

“Wanamapinduzi wanaweza kuuliwa, lakini fikra za kimapinduzi zitaendelea kuishi daima”

Hapo alikuwa akinukuu maneno ya Mwanamapinduzi maarufu Duniani, Ernesto Che Guevara ambaye aliwahi kusema..

“Revolutionaries and individuals can be murdered, but ideas never die.”

Thomas Sankara alifariki Oktoba 15 mwaka 1987 baada ya kupinduliwa na Blaise Compaore kuchukuwa utawala nchini Burkina Faso kwa muda wa miaka 27.

Inafahamika kwamba, kwa mara ya kwanza mwaka 1997, familia ya marehemu Thomas Isodoré Noël Sankara, ilifikisha ombi la kutaka mwili wa Sankara ufukuliwe ili ufanyiwe uchunguzi.

Taarifa zinafahamisha kuwa serikali ya Blaise Compaore ilitupilia mbali ombi kutoka familia ya Thomas Sankara la kutaka kufanyike uchunguzi kuhusu kifo cha Sankara.

Kwa mujibu ya ripoti ya kifo cha Thomas Sankara, serikali ilifahamaisha kuwa Thomas Sankara alifariki kifo cha kawaida.

Familia ilitaka kufahamu kama ni kweli katika kaburi hilo ndipo mwili wa Thomas Sankara ulipohifadhiwa.

“Imenukuliwa”