DC JUMA HOMERA AFUNGA MAFUNZO YA JESHI LA AKIBA KATA YA KALULU WILAYANI TUNDURU

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe. Juma Zuberi Homera amewataka wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la Akiba kujitolea kutumia mafunzo waliyoyapata kwa kuwa wazalendo katika shughuli za umma.

Hayo ameyazungumza wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya wahitimu 50 wa jeshi la Akiba yaliyofanyika kijiji cha rahaleo kilichopo Kata ya kalulu wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.

Mkuu wa wilaya amesema kuwa mafunzo ya kijeshi yatumike kwa uzalendo na wahitimu wote serikali itawapa kipaumbele katika masuala yanayohusu ulinzi na usalama kwa kuwa jeshi la wananchi na jeshi la polisi halipo kila mahali lakini kwa kuwatumia wahitimu wa jeshi la akiba serikali inakuwa karibu zaidi na wananchi.

Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Mhe. John Pombe Magufuli ameamua kurudisha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) kwa kuwa anatambua umuhimu wake kwa Taifa letu.

Aidha, Amewataka wahitimu wakatimize wajibu wao wa kuwa raia wema na kuwa walinzi kwa kupitia mafunzo ya ulinzi na usalama waliyoyapata huku akieleza kuwa Serikali inapambana na changamoto za kukabiliana na wahalifu hususani maeneo ya mipakani na wao wanaweza kutumika kuisaidia serikali.

Mwisho Dc Homera aliahidi wananchi kuwa jumatano ya tarehe 15/11/2017 atakabidhi bati 70 kwa shule ya msingi kalulu na atamuagiza mganga mkuu wa wilaya amlete mhudumu wa afya ndani ya siku saba katika zahanati ya Mbungulaji.

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*