DC HAPI ASHUSHA NEEMA KWA WANANCHI KUNDUCHI AHITIMISHA MGOGORO WA ARDHI, KUWAFUTA MACHOZI WANANCHI

Mkuu wa Wilaya ya Kindoni Mhe Ally Hapi leo ametangaza msimamo wa serikali ya wilaya ya Kinondoni kuwa wananchi wa Kunduchi Mecco na mji mpya Kata ya Kunduchi waliokuwa na hofu ya kuondolewa kuwa hawataondolewa na kwamba badala yake makazi yao yatapimiwa viwanja na watamilikishwa rasmi.

Uamuzi huo umekuja baada ya mvutano wa miaka mingi baina ya manispaa ya Kinondoni na wananchi hao waliovamia eneo hilo ambalo awali lilitengwa kwa ajili ya machimbo ya kokoto. Katika mvutano huo ulioibua kesi mbili zilizoendeshwa kwa muda mrefu na hatimaye manispaa kushinda kesi hizo.

Uamuzi umefikiwa kuwa Manispaa ya Kinondoni haitawavunjia na kuwaondoa wananchi hao wapatao zaidi ya 3000 waliojenga eneo hilo. Badala yake eneo hilo litapimwa ili kupanga vema mji na kuruhusu maeneo ya huduma za msingi za jamii kama barabara, shule, afya na zahanati kutengewa maeneo.

Akiambatana na Meya wa manispaa hiyo Benjamin Sitta pamoja na Kaimu Mkurugenzi, Mh. Hapi ameeleza kuwa serikali ya wilaya itaendelea kumaliza migogoro ya ardhi wilayani humo na kwamba wananchi waendelee kuiunga mkono na kuipa ushirikiano.

Uamizi huo umepokewa kwa shangwe kubwa na wananchi wa Kunduchi walioamua kumuamuru dereva azime gari la DC HAPI na kulisukuma huku wakina mama wakilifuta vumbi kwa kanga kama ishara ya kufurahia uamuzi huo.

“Leo natangaza rasmi uamuzi wa serikali ya wilaya kuwa hamtaondolewa hapa.Badala yake mtapimiwa na kumilikishwa kihalali ili mpewe hati.”
Alisema DC Hapi.

Akishukuru kwa niaba ya wananchi wake, diwani wa kata hiyo Mh. URIO ameishukuru serikali kwa uamuzi huo na kwamba wananchi wake wataendelea kuiunga mkono.