DC HAPI AANZA UTATUZI MGOGORO WA ARDHI MABWEPANDE, MBOPO,MJI MPYA

*ATOA SIKU 30 MASHAMBA YOTE KUHAKIKIWA

*AWATAKA WANAOTISHIA WENZAO AMANI KUSAKWA

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh Ally Hapi ameendelea na utatuzi wa migogoro mikubwa ya ardhi ambapo jana amefanya mkutano na wananchi katika eneo la Mabwepande, Mbopo na Mji mpya.

Mkutano huo ambao kwa mara ya kwanza baada miaka mingi umewakutanisha wamiliki wa mashamba na wanaotuhumiwa kuwa wavamizi umefanyika katika mtaa wa Mbopo eneo la Mabwepande.

Akielezea dhamira yake kwa wananchi wa Kinondoni,DC Hapi amesema dhamira yake ni kumaliza mgogoro huo ambao kwa muda mrefu umesababisha uadui, chuki na uvunjifu wa amani miongoni mwa pande zote mbili hali iliyofanya wenye mashamba kushindwa kufika kwenye mashamba yao.

“Nataka mgogoro huu ufike mwisho,tena kwa amani na utulivu ili kila mmoja apate haki yake.Tumeamua kufanya uhakiki wa kina na kuyapima mashamba yote ili yawe katika viwanja, jambo ambalo litawezesha upangaji na uendelezaji mzuri wa mji wetu huku tukitenga huduma muhimu za jamii. Kazi hiyo ndio wajibu tuliopewa na Mh. Rais Dr. John Pombe Joseph Magufuli, lazima tuifanye sasa ili kila mmoja ajue hatima yake kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae.”
Alisema Hapi.

Mkuu huyo wa wilaya metoa siku thelathini (30) kwa wataalam wa Mipangomiji na Ardhi Manispaa Ya Kinondoni kuhakikisha wanafanya uhakiki wa wenye mashamba na wakazi wote katika maeneo hayo huku kila mmoja akitakiwa kuwasilisha nyaraka zake halali za umiliki wake.

Amesema uhakiki huu ni katika harakati za kutatua mgogoro uliopo kwa sasa na hasa ikizingatiwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Mh John Pombe Magufuli imadhamiria kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa migogoro ya Ardhi na kwamba mkakati wa Wilaya uliopo ni kufuta mashamba na kuwa na viwanja vilivyopimwa katika Manispaa.

“Tunataka tupange mji wetu katika viwanja ili kila mmoja aweze kuendeleza eneo lake, na kama hawezi kuendeleza aliachie.”amesema DC.

Mh. Hapi amewataka wakazi wa maeneo hayo kuwa watulivu,kudumisha amani na kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa wataalam wa Mipangomiji ili uhakiki uweze kufanikiwa. Aidha amewataka kuvifichua vikundi vya uhalifu vinavyopiga na kutisha watu wenye mashamba na kuuza maeneo yao hovyo.

“Hao wanaofanya uhalifu huo wa kupiga watu, kuuza mashamba yao hovyo na kuvuruga amani sitawavumilia.Jeshi la Polisi nawaagiza muwasake na kuwakamata wote.” Alisema

Ameongeza kuwa kila mwenye shamba ahakikishe siku ya uhakiki anakuwa na nyaraka zake zote zinazomtambulisha uhalali wake na kila mtu asimame kwenye eneo lake.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya amesimamisha uendelezaji wa aina yeyote katika kipindi hiki ili kupisha zoezi la uhakiki.
Wananchi wa Mabwepande, Mbopo na Mji mpya wamemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya na kumkabidhi majina ya vikundi vya uhalifu vinavyohatarisha amani, kuuza maeneo ya watu hovyo, kukata miti na kuwapiga wamiliki wake wanapokwenda kuyatazama au kuyaendeleza.