DANGOTE KUONGOZA MKUTANO WA MABILIONEA WA DUNIA NCHINI

ALHAJI Aliko Dangote ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa zaidi ya 200 kutoka mataifa mbalimbali duniani wanaotarajiwa kutua nchini kwa ajili ya mkutano utakaozungumzia fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali zikiwamo za utalii, biashara na uzalishaji viwandani.

Mkutano huo utafanyika nchini kwa siku mbili kuanzia Novemba 8 na umeandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), kwa kushirikiana na kampuni inayoandaa maonyesho ya kimataifa na Huduma za Mikutano Afrika (IECS).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wanachama wa TPSF, Luis Akaro, alisema mkutano huo utatoa fursa ya kipekee kwa Tanzania katika kuvutia uwekezaji.

Alisema katika mkutano huo, Dangote ambaye ni mfanyabiashara tajiri barani Afrika, atahamasisha na kutafuta watu watakaowekeza kwenye sekta ya kilimo nchini.

“Mkutano huo utazungumzia fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwamo utalii, biashara na uzalishaji viwandani. Washiriki mbalimbali ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuzungumza kwenye mkutano huu wa kimataifa,” alisema.

Pia alisema kuwa katika siku zijazo, Tanzania itakuwa na mazingira mazuri zaidi ya kibiashara kutokana na kuwa na sera nzuri za mageuzi ya kifedha.

“Serikali ya awamu ya tano inaendelea kuboresha mazingira mazuri ya biashara. Ziko hatua madhubuti zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Rais John Magufuli kupambana na rushwa na ufisadi ambazo zinapongezwa na dunia kama njia inayoelekeza Tanzania kwenye lengo lililo sahihi,” alisema.

Pia alisema ujenzi wa uwanja mpya wa ndege wa kimataifa unaoelekea kukamilika jijini Dar es Salaam, upanuzi wa Bandari ya jiji hilo (Dar es Salaam), ujenzi wa reli ya kisasa yenye kiwango cha standard gauge, pamoja na kuanzishwa maeneo maalum ya kiuchumi, kumeifanya Tanzania kuwa kivutio cha uwekezaji.

Mkurugenzi Mwenza wa kampuni ya IECS, John Suddrey, alisema washiriki kwenye mkutano huo watatoka nchi mbalimbali zikiwamo Norway, Canada, Marekani, Uingereza na wengine watatoka barani Asia na Afrika.

Katika hatua nyingine, Suddrey alisema kuwa baada ya mkutano huo, kutakuwa na shindano la wajasiriamali ambao watatakiwa kuandaa wazo la biashara na mshindi atapata dola za Marekani 1,000.

Alisema shindano hilo ni kwa ajili ya wajasiriamali kutoka Tanzania, Kenya na Uganda na kwamba, ili kushiriki shindano hilo, watu watatakiwa kutembelea tovuti ya www.investintanzaniaconference.co

Chanzo: IPP Media