ASKOFU MKUU ZANZIBAR: JPM AUNGWE MKONO, AMEONYESHA NJIA.

Askofu mkuu wa jimbo katoliki Zanzibar mhashamu askofu Augustine Shao ametoa rai kwa watanzania kuunga jitihada anazozionyesha rais wa awamu ya tano Mh Dr John Pombe Magufuli katika kurekebisha mambo muhimu kwa maendeleo ya taifa.


Askofu shayo ameyasema hayo leo katika ibada iliyofanyika katika kanisa la mtakatifu Joseph parokia ya Minara miwili mjini zanzibar ambayo ilihudhuriwa pia na Mheshimiwa Rais na ujumbe wake.

Askofu Shao ameeleza kwamba mapambano ya mheshimiwa rais ni yenye kuwa na mguso wa moja kwa moja kwa maisha ya watanzania na hivyo ipo haja ya kila mtanzania kuunga mkono jitihada hizo.

“Mapambano dhidi ya rushwa kwa mfano ni mapambano yetu, rais ameonyesha njia ni lazima tumuunge mkono” alisema Askofu Shao.

Kwa upande wake mheshimiwa rais mara baada ya kumalizika kwa ibada hiyo amemshukuru askofu Shao kwa mahuburi hayo huku akisisitiza kwamba serikali ya awamu ya tano imejipambanua kupambana na rushwa katika ngazi zote ili kuhakikisha wananchi wananufaika na matunda ya rasilimali zao kama ilivyokua dira ya waasisi wa taifa hili.