NAIBU WAZIRI ATOLEA UFAFANUZI KUHUSU TSSF

Na John Marwa
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh.Ole Nasha ametolea ufafanuzi kuhusiana na suala la Shirika lisilo la kiserikali ya TSSF lililotangaza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Akifafanua Mh.Ole Nasha amesema,Wizara ya Elimu haina taarifa ya kuwepo kwa shirika hilo na haitawajibika kwa lolote na amewataka wananchi watakaotumia huduma hiyo, kuwa waangalifu.

“Tutakutana na hili shirika la TSSF Jumanne ijayo, tunataka tulijue kwa ukaribu zaidi kama mdau wa sekta tunayosimamia” amesema Waziri.

Aidha ameongeza kuwa, ni wazi kwamba taasisi yenye uwezo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi 50,000 si taasisi ndogo lama watu wanavyofikiria na kwamba katika hali ya kawaida, Wizara ingekuwa inaifahamu na kushirikiana nayo kikamilifu.

“Kwa bahati mbaya TSSF haijawahi kujitambulisha kwa Wizara jambo ambalo linafanya ufahamu wetu kuhusu tasisi hiyo kuwa mdogo. Ndio tumetoa tahadhari kwa umma ili madhara yakitokea ifahamike kuwa si mshiriki wa Wizara”. amesema Mh.Nasha.

“Twendeni taratibu ndugu zangu, hakuna kiongozi yoyote wa serikali anayefurahia mwanafunzi yoyote kukosa mikopo, Bajeti yetu ya mikopo kwa mwaka huu ni shilingi billion 427 kwa vyovyote vile haitoshi ndio maana tunahakikisha kwamba wale wenye mahitaji zaidi ndio wanapewa kipaumbele. Kwa hili Bodi ya mikopo imejitahidi sana.

Waziri amekiri kwa kusema kuwa, katika kuchakata maombi makosa madogomadogo hutokea, ndio maana kuna nafasi ya kukata rufaa na kwamba baadhi ya wanafunzi wanakosa mikopo kwa sababu ya kutojaza fomu ipasavyo au kutoleta viambatisho husika.

Amesema, kuna mipango ya kuongeza uwezo wa Bodi ya Mikopo kuwafikia wanafunzi wengi zaidi. Hii inaenda sambamba na kuhakikisha wale ambao tayari wamepata mikopo wanalipa madeni yao kwa wakati.

Ameongeza kuwa, hata hivyo bado wizara inaendelea kuchunguza taasisi husika kwa umakini na itatoa taarifa kwa umma kadri mambo mapya yatakapojitokeza.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk.Donat Salla amekanusha tuhuma dhidi ya taasisi hiyo kwamba ni matapeli na ameonesha vithibitisho kupitia ukurasa wao wa Facebook.

Pia amekiri walipokea ugeni toka wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia siku ya Ijumaa

Katika maelezo yao wasema kuwa, wana kiasi cha Sh.Billion 12 kwa ajili ya mikopo na kwamba, wamesaini mkataba na fundraising agency ya Marekani ili waweze kupata hizo fedha.

Hata hivyo inadaiwa kuwa, kwa hapa nchini tayari TSSF wanachukua sh.elfu 30 kwa kila mwombaji mikopo.

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*