FAHAMU TABIA ZA KUZIEPUKA WAKATI UNAPOKULA CHAKULA

Imeandikwa na Augustino Chiwinga.

Ni ukweli kwamba wazazi wetu wa kiafrika wametufunza tamaduni na ustaarabu mbalimbali lakini kwenye suala la kula kistaarabu (Table Manners) walichemka kutufunza.

Ukitaka kulijua hilo fuatilia katika migahawa uone jinsi watu wanavyokula bila ya kuzingatia ustaarabu.

Sasa Leo nazianisha tabia ambazo unatakiwa kuziepuka wakati wa chakula hususani unapokula na watu wengi.

1.KUBEUA/KUCHEUA.

Kubeua au kuchuea ni tabia mojawapo ambayo inatakiwa kuepukwa wakati wa kula.

Kubeua/kucheua ni kile kitendo cha kutoa muungurumo wa hewa kutoka tumbo wakati wa kula. Hiyo sauti huwa inaambatana na harufu kali kutoka tumboni hovyo haifai kufanya hivyo mbele za watu.

Unapotaka kubeua /kucheua ni vyema ukasogea pembeni kidogo ili kuepuka kuwatia kinyaa wenzio unaokula nao.

2.KUONGEA NA KUCHEKA.

Ni ukweli kwamba wakati wa kula mtu hatakiwi kuongea au kucheka bila ya ulazima wa kufanya hivyo.

Kwani kuongea na kucheka kutasababisha mabaki ya chakula yaliyosagwa na meno kuonekana kwa mwenzako au wenzako unaokula nao hali ambayo inaweza kupelekea kupata kichefu chefu au wengine kushindwa kuendelea kula.

Hivyo basi inashauriwa kwamba kama unakula na ukalazimika kuongea basi jitahidi kwanza umeze chakula,kisha unywe maji ndipo ufungue mdomo kuongea napo haitakiwi kufungua mdomo mpaka mwisho.

3.KUJICHOKONOA NA KIJITI (TOOTHPICK)

Unapokula vyakula vyenye asili ya nyama kama vile samaki ni kawaida mabaki ya vipande vya nyama kubaki katikati ya meno.

Hapo ndipo watu wengi wanapotumia vijiti kuyaondoa mabaki hayo.Lakini katika kufanya hivyo watu wengi huwa wanakosea wanajichokonoa kwa kutanua mdomo bila kujiziba na kitu chochote, huo sio ustaarabu kwani hakuna anayependa kuyaona mabaki ya chakula ukiyatoa katika meno yako.

Ustaarabu inatakiwa iwe hivi chukua kijiti chako kisha tumia kiganja chako cha kushoto kuziba mdomo kisha ingiza kijiti kwa mkono wa kulia kisha uanze kuondosha mabaki hayo.

Njia hii ni nzuri na inasaidia kutokumkera mwenzio ambaye unakua unakula nae maeneo hayo.

Pia tabia ya kutumia vidole kuondoa mabaki hayo sio uungwana na ustaarabu kabisa.

4.KUJIFUTA MDOMO.

Watu wengi wakiwa wanakula au baada ya kula huwa wanapendela kujifuta mdomo kwa mikono yao mitupu.

Tabia hiyo sio nzuri tafuta kitambaa au karatasi laini kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.

Ukiwa unakula kuna chakula kinaweza kubakia katika midomo yako ,hivyo jitahidi kila mara uwe unajipangusa mdomo kwa tissue au kitambaa laini kabla ya kumaliza kula chakula chako.

5.KUVUTA CHAI.

Watanzania wengi hua hatunywi chai bali tunavuta chai.

Chunguza katika watu watatu wanaokunywa chai lazima utasikia wanakunywa chai kwa mtindo wa kuvuta.Hapo ndipo utasikia sauti za ajabu kama vile “tsuuu””brrrr” na nyinginezo .Hakika tabia hii inakera sana.

Ustaarabu ni kwamba unapokunywa chai shika kikombe chako sawa sawa kisha kiinue kukipeleka mdomoni kisha taratibu imimine katika mdomo wako.Hapo hutoweza kusikia sauti ya kuvutwa kwa chai.

Tabia ya kuvuta chai inaweza kumkera jirani yako .

6.KATA KUCHA ZAKO.

Hakuna kitu kinatia kinyaa kama unapokula na mtu mwenye kucha ndefu halafu nyeusi .

Hakika hamu ya chakula inaondoka hapo hapo.

Jitahidi kuziweka kucha zako katika hali ya usafi kwa kuzikata na kuzisafisha mara kwa mara.

7.MAJI YA KUNAWA.

Miaka ta zamani tulikua tunatumia sufuria au beseni moja kunawia familia nzima pale tulipokua tunataka kula.

Lakini siku hizi mambo yamebadilika , ustaarabu ni kutumia maji ya kuchuruzika na sabuni.

Tabia ya kutumia maji kwenye chombo kimoja inaweza kusababisha kuletaa magonjwa kama vile kipindupindu kwa sababu mtu wa kwanza ndiye anayekua amenawa maji safi hawa wengine wanakua wananawa uchafu wa wenzao.

 

8.KUTEMA MATE

Epuka kutema mate jirani na eneo mnalokula chakula.

Kutema mate kunaweza kusababisha kinyaa kwa watu waliokuzunguka

Unapotaka kufanya hivyo ni bora ukasogea pembeni kabisa kisha ukatema.

Kwa leo naishia hapa, tukutane tena siku nyingine, nawatakia mapumziko mema ya wikiendi.

 

 

Augustino Chiwinga.

0756 810804